MARIA KUPALIZWA MBINGUNI
MATANDA RICHARD TESHA
Sikukuu ya Kanisa Katoliki inayoadhimishwa kila
mwaka tarehe 15 Agosti. Inatokana na dogma iliyotangazwa na Papa Pius XII kwa hati Munificentissimus Deus ya tarehe 1 Novemba 1950 baada ya kusikiliza maoni ya maaskofu wote.
Fundisho hilo la imani ni kwamba Bikira Maria, mama wa Yesu, alipomaliza maisha yake duniani
alichukuliwa mwili na roho mbinguni, ashiriki mapema utukufu wa Mwanae mfufuka kama
alivyoshirikiana naye toka mwanzo hata mwisho wa maisha yake. Fundisho hilo
linalingana na lile la Waorthodoksi, ingawa hao hawajalitangaza kuwa
dogma. Tarehe hiyo wao wanaadhimisha ya Kulala kwa Bikira Maria.
Umoja wa msimamo huo upande wa
mashariki na wa magharibi wa Kanisa unatokana na mapokeo ya karne za kwanza za Ukristo, yanayoshuhudiwa na mababu wa Kanisa kama vile Efrem wa Syria, Timoteo wa Yerusalemu, Epifanio wa Salamina, Yohane wa Damasko.
Jina asili kwa Kiaramu ni מרים, Maryām
lenye maana ya "Bibi"; watafsiri wa kwanza wa Biblia ya Kiebrania wanaojulikana
kama Septuaginta (LXX) waliliacha kama lilivyo
wakiandika kwa Kigiriki Μαρίαμ, Mariam,
au walilifupisha wakiandika Μαρία, Maria.
Kwa heshima, mama wa Yesu anatajwa kwa kawaida kwa kutanguliza sifa yake
mojawapo, hasa Bikira.
Mapokeo ya karne ya 2 (Injili ya Yakobo) kuhusu Bikira Maria yanasema
alikuwa binti pekee wa Yohakimu na Ana. Lakini habari
muhimu zaidi ni zile zinazopatikana katika Biblia ya Kikristo.
BIKIRA MARIA KATIKA BIBLIA
Biblia inashuhudia kuwa umuhimu wa watu
unatofautiana
Maandiko
matakatifu yanawasifu watu mbalimbali kutokana na jinsi walivyomuamini Mungu na kutenda
makuu kwa ajili ya taifa lake.
Abrahamu alimuamini
Mungu akawa tayari kumtolea sadaka mwanae Isaka, tukio
lililomfanya apate baraka ya pekee ya
kuwa baba wa waamini (Mwa 22:15-18).
Yosefu, mwana mpenzi
wa Yakobo, alikuwa
mwaminifu hata akaliokoa taifa lisiangamie kwa njaa (Mwa 50:20).
Musa ndiye mkombozi wa taifa la Mungu katika Agano la Kale: aliongoza Israeli kutoka
[[utumwani Misri akalipatia sheria kutoka kwa
Mungu katika mlima Sinai. Maandiko ya
Agano la Kale yanakiri, “Wala hajainuka kiongozi kama alivyokuwa Musa” (Kumb
34:10-12).
Waliofuata ni Yoshua, Debora, Gideoni, Ruthu, Samweli, wafalme Daudi na Solomoni, manabii Eliya, Isaya, Yeremia, Ezekieli na wengineo.
Mwishoni Yesu Kristo akamsifu Yohane Mbatizaji akisema, “Ni
mkuu kati ya uzao wa wanawake” (Lk 7:24-28).
Elizabeti, mama wa
Yohane, alijiona hastahili kutembelewa na Bikira Maria, Mama wa Yesu, akamuita,
“Mama wa Bwana wangu” (Lk 1:43).
Bikira Maria si
mtu wa ziada katika mpango wa Mungu bali ni
mshiriki mkuu wa ukombozi wa binadamu. Maria
amechangia wokovu kwa kukubali mpango wote wa Mungu aliyetaka amzae Mwanae,
amlee na kumfuata kiaminifu hadi msalabani, aliposhiriki kumtoa kama sadaka ya
kutuokoa. Msimamo wake ulikuwa mmoja tu: “Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na
iwe kwangu kama ulivyosema” (Lk 1:38).
Tukichunguza nafasi yake katika fumbo hilo, tunaweza
kukiri pamoja naye kuwa ni Mwenyezi Mungu aliyemtendea makuu (Lk 1:49), kwa
kuwa, “Mtu hawezi kuwa na kitu asipopewa na Mungu” (Yoh 3:27).
Yale yote ambayo Wakristo wengi
wanayasadiki kuhusu Bikira Maria, hakujipatia bali alijaliwa na Mwenyezi Mungu
huku akiitikia kwa hiari fumbo la
mpango wake.
UTABIRI KUHUSU
BIKIRA MARIA
Biblia inatupatia utabiri uliotolewa na
Mungu mwanzoni mwa historia kuhusu mwanamke atakayemshinda
nyoka wa kale (Shetani): “Nitaweka
uadui kati yako na huyu mwanamke, kati ya uzao wako na uzao wake; huo
utakuponda kichwa chako” (Mwa 3:15). Juu ya [[Eva wa kale, ambaye alidanganywa
na kuangushwa na Shetani atende dhambi, imesemwa: “Adamu akamwita mkewe jina lake
Hawa, kwa kuwa ndiye aliye Mama wa walio hai” (Mwa 3:20). Hata hivyo Adamu na
Eva wa kale wametuletea kifo (Rom 5:12). Mababu wa Kanisa wanamtazama
Bikira Maria kama Eva mpya aliyemshinda Ibilisi na kuwa mama
wa wote walio hai. Yesu, aliye Adamu mpya, alipokuwa
anakamilisha sadaka ya ukombozi pale msalabani alimfanya Mama
yake awe Mama wa waliokombolewa kwa kumkabidhi mwanafunzi, tena yule
aliyempenda zaidi. “Penye msalaba wake Yesu walikuwa wamesimama mamaye, na umbu
la mamaye, Mariamu wa Kleopa, na Mariamu Magdalene. Basi Yesu alipomwona mama
yake, na yule mwanafunzi aliyempenda amesimama karibu, alimwambia mama yake,
“Mama, tazama, mwanao”. Kisha akamwambia yule mwanafunzi, “Tazama, mama yako”.
Na tangu saa ile mwanafunzi yule akamchukua nyumbani kwake. (Yoh 19:26-27).
Utabiri mwingine ulisema, “Tazama Bikira atachukua mimba, atazaa mtoto mwanamume, naye atamuita
jina lake Emanueli, yaani Mungu
pamoja nasi” (Isa 7:14). Dondoo hilo linalinganishwa na Lk 1:34-35, “Mariamu
akamwambia malaika, Litakuwaje
neno hili, maana sijui mume? Malaika
akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu akakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika
kama kivuli. Kwa sababu hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu”. “Imba, ee
binti Sion, piga kelele,
ee Israeli, furahi na kushangilia kwa moyo wako wote, ee binti Yerusalemu. Mfalme wa Israeli,
naam, yeye Bwana yu katikati
yako” (Sef 3:14-15). Dondoo hilo linalinganishwa na Lk 1:28: “Malaika akaingia
nyumbani mwake akamwambia, ‘Furahi Maria, umejaliwa neema kubwa, Bwana yu
pamoja nawe’”. “Umebarikiwa wewe katika kila hema la Yuda na katika kila
taifa, nao wanaposikia jina lako watafadhaika. Imani yako haitatoka
mioyoni mwa watu wanaoukumbuka uweza wa Mungu milele” (Yudithi 14:7; 15:9). Dondoo hilo linalinganishwa na Lk
1:42, “Akapaza sauti kwa nguvu akasema, ‘Umebarikiwa wewe kuliko wanawake wote,
na yeye utakayemzaa amebarikiwa’”.
Bikira Maria ni fumbo la ajabu alilolifanya Mungu katika
mpango wa wokovu kwa ajili yake
na kwa ajili yetu. Jamaa yake Elizabeti alimpongeza tena akiongozwa na Roho
Mtakatifu, “Heri yako wewe
uliyesadiki kwamba yatatimia yale uliyoambiwa na Bwana” (Lk 1:45).
Hivyo manabii mbalimbali kwa mwanga wa Roho Mtakatifu
walimuagua Maria kwa heshima. Mambo yaliyotabiriwa katika Agano la Kale
yalitimia katika Agano Jipya: ukombozi ulianza Bikira Maria
alipokubali kwa imani fumbo la umwilisho wa Mwana wa
Mungu. Bikira Maria hakuwa “chombo” tu kilichotumika bila ya kuelewa, bali
alikuwa mshiriki huru wa kazi ya ukombozi ya Mwanae, kwa kuwa alipopashwa
habari na malaika alikubali kwa hiari mpango wa Mungu akisema, “Mimi ni
mtumishi wa Bwana, na iwe kwangu kama ulivyonena” (Lk 1:38).
BIKIRA MARIA KATIKA MAISHA YA YESU
Yesu, kama mtu yeyote mcha Mungu, aliwaheshimu na kuwatii
wazee wake: “Basi, akarudi pamoja nao Nazareti, akawa
anawatii” (Lk 2:51).
Ishara ya kwanza
kwenye maisha ya
hadhara ya Yesu iliongozwa na Bikira Maria katika arusi ya Kana ya Galilaya, akisukumwa na
huruma kwa wenye
shida: kwa ombi lake Yesu aligeuza maji kuwa divai, na wanafunzi
wake wakamwamini. Yohane alisimulia hivi, “Siku ya tatu palikuwa na arusi huko
Kana, mji wa Galilaya; naye mama yake Yesu alikuwapo. Yesu naye alikuwa
amealikwa arusini pamoja na wanafunzi wake. Hata divai ilipowatindikia, mamaye
Yesu akamwambia, ‘Hawana divai’. Yesu akamwambia, ‘Mama tuna nini mimi nawe?
Saa yangu haijawadia’. Mamaye akawaambia watumishi, ‘Lo lote atakalowaambia,
fanyeni’. Basi kulikuwako huko mabalasi sita ya mawe, nayo yamewekwa huko kwa
desturi ya Wayahudi ya kutawadha, kila moja lapata kadiri ya nzio mbili tatu.
Yesu akawaambia, ‘Jalizeni mabalasi maji’. Nao wakayajaliza hata juu.
Akawaambia, ‘Sasa tekeni, mkampelekee mkuu wa meza’. Wakapelekea. Naye mkuu wa
meza alipoyaonja yale maji yaliyopata kuwa divai, (wala asijue ilikotoka,
lakini watumishi walijua, wale walioyateka yale maj), yule mkuu wa meza
alimwita bwana arusi, akamwambia, ‘Kila mtu kwanza huandaa divai iliyo njema;
hata watu wakiisha kunywa sana ndipo huleta iliyo dhaifu; wewe umeiweka divai
iliyo njema hata sasa’. Mwanzo huo wa ishara Yesu aliufanya huko Kana ya
Galilaya, akaudhihirisha utukufu wake, nao wanafunzi wake wakamwamini. (Yoh
2:1-12).
Bikira Maria anasifiwa kwanza kwa imani yake kuu kabisa,
kuliko kwa kumchukua Yesu tumboni tu. Yesu alitaka kuwainua wasikilizaji wake
wafuate mambo ya roho kuliko ya mwili. “Basi, mtu mmoja akamwambia, ‘Mama yako
na ndugu zako wako nje, wataka kusema nawe’. Lakini Yesu akamjibu huyo mtu
aliyemwambia hivyo, ‘Mama yangu ni nani, na ndugu zangu ni akina nani?’ Kisha
akanyosha mkono wake juu ya wanafunzi wake akasema, ‘Hawa ndio Mama yangu na
ndugu zangu, maana yeyote anayefanya anavyotaka Baba yangu aliye mbinguni, huyo
ndiye kaka yangu na dada yangu na mama yangu’” (Math 12:46-50). Vilevile,
wakati wa utume wake,
alimsikia “mwanamke mmoja katika lile kundi la watu akisema, ‘Hongera kwa
mwanamke aliyekuzaa na kukunyonyesha’. Yesu akamjibu, ‘Barabara, lakini heri
yake zaidi yule anayelisikia Neno la Mungu na kulishika’” (Mk 11:27-28).
BIKIRA MARIA ALIVYOSHIRIKI MATESO YA
YESU
Katika kumfuata Mwanae Bikira Maria alitabiriwa wazi na
mzee Simeoni uchungu kama upanga utakaopenya moyo wake, “Tazama
huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi katika Israeli, na kuwa ishara
itakayonenewa. Nawe mwenyewe uchungu ulio kama upanga utauchoma moyo wako” (Lk
2:34-35).
Bikira Maria alishiriki kwanza mateso ya ukimbizi huko Misri kwa
lengo la kumficha Mwanae asiuawe na Herode Mkuu, “Hivyo Yosefu aliamka akamchukua mtoto
pamoja na Mama yake akaondoka usiku akaenda Misri akakaa huko mpaka Herode
alipokufa” (Math 2:14-15).
Bikira Maria alishuhudia hatua kwa hatua kuteswa kwa
Yesu; wanafunzi walipokimbia au kumtazama kwa mbali, yeye alikuwa karibu akaona
vema kila teso lililompata Mwanae. Kutokana na fungamano la upendo wa ajabu
lililokuwepo kati ya Yesu na Mamaye, alipoyashuhudia yote aliteseka sana katika
moyo wake safi, kiasi kwamba Bernardo wa
Klervoo akasema, “Msalaba wa Yesu uliwasulubisha wote wawili, Yesu mwilini na Mama
yake moyoni”. Uaguzi wa mzee Simeoni ulitimia hivyo.
Kadiri ya mtume Paulo kuteseka ni kutimiliza yaliyopungua
katika mateso ya Kristo kwa ajili ya Kanisa, “Na sasa
nafurahi kuteseka kwa ajili yenu, maana kwa mateso yangu hapa duniani nasaidia
kukamilisha kile kilichopungua bado katika mateso ya Kristo” (Kol 1:24). “...
maana tukiyashiriki mateso yake Kristo, tutaushiriki pia utukufu wake” (Rom
8:17b).
Pale msalabani Bikira Maria, kwa njia ya mtume Yohane alifanywa Mama
wa wote wanaompenda Mwanae; kisha kumzaa pasipo uchungu Bwana wa uzima, pale alituzaa
sisi kwa uchungu wa kutisha uliotokana na kumuona Mwanae akifa msalabani. Hata
hivyo Bikira Maria aliendelea kumuamini Mwanae aliyeonekana ameshindwa.
BIKIRA MARIA BAADA YA KIFO CHA YESU
Bikira Maria alikuwepo hapo mwanzo wa Kanisa, akilivutia
zaidi Roho Mtakatifu kwa sala yake. “Hao
wote walikusanyika pamoja kusali, pamoja na wanawake kadha wa kadha, na Maria
Mama yake Yesu na ndugu zake” (Mdo 1:14).
Yesu alisema, “Ninayo bado mengi ya kuwaambieni, ila kwa
sasa hamwezi kuyastahimili, lakini atakapokuja huyo Roho wa ukweli atawaongoza
kwenye ukweli wote” (Yoh
16:12-13). Kwa msaada wa Roho Mtakatifu heshima kwa Bikira Maria ilienea katika
Kanisa lote tangu zamani kabisa kadiri ya utabiri wake kuwa ataheshimiwa na
vizazi vyote, “Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma mtumishi wake mdogo, hivyo
tangu sasa vizazi vyote wataniita mwenye heri” (Lk 1:48).
Kuna mafundisho makuu manne kumhusu Bikira Maria ambayo
ni lazima kila Mkatoliki ayasadiki kutokana na ufunuo wa Mungu: 1. B. Maria mkingiwa
dhambi ya asili 2. B. Maria Mama wa Mungu 3. B. Maria Bikira daima 4. B. Maria kupalizwa
mbinguni mwili na roho
1.
Mkingiwa Dhambi ya Asili
Malaika alimsalimia Maria “umejaa neema” (Lk 1:28) maana
ndiye tunda bora la ukombozi ulioletwa na Yesu. Ni imani ya Wakatoliki kwamba
kwa stahili za Mwanae alikingiwa asirithi kwa wazazi dhambi ya asili na madonda
yanayotokana nayo, wala asitende dhambi maisha yake yote. Kwa maneno mengine,
Bikira Maria tangu atungwe mimba Mungu alimkinga na kila doa la dhambi kwa
kutazamia stahili za Yesu Kristo
aliye Mkombozi wa binadamu wote. Ndiye aliyekombolewa kwa namna bora kushinda
viungo vyote vya Kanisa. Maisha yake yote hakutenda dhambi hata moja. Mapokeo
ya mashariki yanamuita “A
Panagia” = “Mtakatifu tu”. Dogma hiyo ilitangazwa na papa Pius IX mwaka 1854, halafu mwaka 1858 Bikira Maria
alijitambulisha kama Mkingiwa kwa Bernadeta
Soubirous huko Lurdi (Ufaransa). Tena mwaka 1917 huko Fatima (Ureno) aliwafunulia Lusia,
Fransisko na Yasinta Marto moyo wake safi usio na doa.
2.
Mama wa mungu
Injili ya Yohane inaanza kwa kishindo, “Hapo mwanzo
kulikuwako Neno, naye Neno
alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu” (Yoh 1:1). Huyo Mungu Mwana alitwaa
ubinadamu katika Bikira Maria akazaliwa mtoto, jina lake Yesu, maana yake Mungu
Mwokozi. Huyo ni binadamu kama sisi katika yote isipokuwa dhambi. Ubinadamu wa
Yesu unategemea Nafsi yake ya
Kimungu: akisema, ‘Mimi’, ni kwa Nafsi yake hiyo. Ndiyo maana aliwaambia Wayahudi, “Kweli
nawaambia, kabla Abrahamu hajazaliwa, nalikuwepo” (Yoh 8:50). “Kama vile Baba alivyo asili ya uhai,
ndivyo alivyomjalia Mwanae kuwa asili ya uhai” (Yoh 5:26).
Mtume Paulo akaeleza, “Wakati maalumu ulipotimia Mungu
alimtuma Mwanae aliyezaliwa na mwanamke” (Gal 4:4). Bikira Maria ni Mama wa
Mungu kwanzia wakati huo: tangu Bikira Maria alipojaliwa kumchukua mimba,
kumzaa, kumnyonyesha na kumlea mtu ambaye kwa asili ni Mungu. Cheo hicho
kimemuinua juu kuliko hata malaika. “Malaika alimwambia, ‘Hicho kitakachozaliwa
kitaitwa Kitakatifu, Mwana wa Mungu’” (Lk 1:35).
Dogma ilitangazwa mwaka 431 kwenye Mtaguso wa Efeso uliomuita
“Mzazi wa Mungu”, ukisema Maria anastahili kuitwa hivyo kwa sababu Mwana wa
milele wa Mungu, ambaye ni Mungu sawa na Baba, alifanyika mtu toka kwake. Akiwa
mja mzito alishangiliwa: “Umebarikiwa wewe katika wanawake, naye mzao wa tumbo
lako amebarikiwa. Limenitokeaje neno hili, hata mama wa Bwana wangu anijilie
mimi?” (Lk 1:42-43). Ungamo hilo la Elizabeti likakamilishwa na Mtume Thoma aliyemuambia
Yesu mfufuka: “Bwana wangu na Mungu wangu!” (Yoh 20:28).
3.
Bikira na Mama
Wakristo na Waislamu wote wanakiri
kuwa Yesu alitungwa bila ya mchango wa mwanamume. La ajabu zaidi katika imani
hiyo ni kwamba hata uzazi wenyewe haukuondoa ubikira wake, bali uliutakasa: ni
Bikira daima. Ingawa akili inasita, ni lazima kukiri na malaika, “Hakuna
lisilowezekana kwa Mungu” (Lk 1:38). Yosefu, ingawa
kisheria alikuwa mume wake, hakutenda naye tendo la ndoa.
Ni imani ya Wakatoliki na Waorthodoksi kuwa Mama wa Yesu
anastahili kuitwa “Bikira daima” kwa sababu alimchukua mimba akiwa bikira,
akamzaa bila ya kupotewa na ubikira, akabaki bikira hadi mwisho wa maisha yake.
Hamu yake ya kuwa bikira hata kisha kuchumbiwa inajitokeza katika jibu alilompa
malaika aliyemtabiria mimba: “Litakuwaje neno hili, maana sijui mume?” (Lk
1:35). Ni kielelezo cha Wakristo ambao Mtume Paulo aliwaandikia: “Nawaonea
wivu, wivu wa Mungu; kwa kuwa naliwaposea mume mmoja, ili nimletee Kristo
bikira safi” (2Kor 11:2), “mpate kumhudumia Bwana pasipo kuvutwa na mambo
mengine” (1Kor 7:35).
Wanaosemwa katika Injili “ndugu zake
Yesu” si watoto wa Bikira Maria, bali ndugu wa ukoo waliokuwa jirani sana na
familia hiyo takatifu. Kama Bikira Maria angekuwa na watoto wengine, Yesu
angekuwa amefanya kosa la kuwanyang’anya Mama yao na kumfanya awe Mama wa mtume
Yohane alipomkabidhi msalabani, “‘Mwana, tazama Mama yako’. Na tangu saa ile
huyo mwanafunzi alimchukua akae nyumbani kwake” (Yoh 19:27).
Katika Agano Jipya yupo Yakobo anayeitwa na mtume Paulo
“ndugu yake Bwana” (Gal 1:19): Yakobo huyo alikuwa maarufu katika Kanisa
la Yerusalemu (Mdo 12:7; 15:13-21; 21:18-20; Gal 2:9). Yakobo huyo si
mtume Yakobo kaka yake Yohane (Lk 6:12-16), bali ni Yakobo ndugu yake Yose na
mama yao kwenye Injili anaitwa “Maria mwingine”, si Maria Mama wa Yesu.
“Walikuwepo pia wanawake waliotazama kwa mbali. Miongoni mwao akiwa Maria Magdalena, Salome na Maria mama
wa akina Yakobo mdogo na Yose” (Mk
15:40). Maria lilikuwa jina la kawaida kwa Wayahudi: akina Maria wakiwa wengi
hivyo, tujue kuwatofautisha kwenye Injili, ambazo zinamtaja Bikira Maria kama
“Mama wa Yesu”.
4.
Kupalizwa mbinguni mwili na roho
Baada ya maisha haya ya duniani Bikira Maria alipalizwa
mbinguni mwili na roho, ishara ya mwanamke mshindi. “Ishara kubwa ikaonekana
mbinguni, ambapo mwanamke aliyevikwa jua, pia na mwezi chini ya miguu
yake, na taji la nyota kumi na mbili
juu ya kichwa chake” (Ufu 12:1). Maneno ya shangilio lake yametimia: Mungu
“amewaangusha wakuu katika viti vyao vya enzi; na wanyonge amewakweza” (Lk
1:52).
Imani hiyo ya mapokeo ya kale, yanavyoshuhudiwa na Mababu
wa Kanisa, ilitangazwa rasmi na Papa Pius XII kwa niaba ya maaskofu wote mwaka
1950.
Kuna ibada za
Mama Bikira Maria zinazoadhimishwa katika liturujia ya Kiroma. Hapa zimepangwa
kulingana na heshima zinavyozidiana:
8 Desemba –
Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili 1 Januari – Bikira Maria Mama wa Mungu 25
Machi – Bikira Maria Kupashwa Habari 15 Agosti – Bikira Maria Kupalizwa
Mbinguni
Juni – Moyo Safi wa Maria 15
Septemba – Mama Yetu wa Huzuni 22 Agosti – Bikira Maria Malkia 7 Oktoba –
Bikira Maria wa Rozari 21 Novemba –
Bikira Maria Kutolewa Hekaluni
11 Februari –
Bikira Maria wa Lurdi 13 Mei – Bikira Maria wa Fatima 16 Julai – Bikira Maria
wa Mlima Karmeli 5 Agosti –
Kutabaruku Kanisa la Bikira Maria 12 Septemba – Jina takatifu la Maria 12
Desemba – Bikira Maria wa Guadalupe
Pia zipo
heshima za binafsi kwa Bikira Maria: mashariki zinatumika tenzi na nyimbo
mbalimbali, k.mf. Akatistos inayomuita “daraja
linalounganisha dunia na mbingu”, “ngazi aliyoiona
Yakobo” “kina kisichochunguzika kwa macho ya malaika” (Mwa 28:12); magharibi]]
anaheshimiwa kwa rozari.
Wakristo
wanaomheshimu Bikira Maria hawamuabudu hata kidogo, lakini wanamtolea heshima
ya juu kuliko watakatifu wengine. Tofauti ni kwamba Mungu tu anastahili
kuabudiwa (kwa Kigiriki, ‘latria’)
watakatifu wanapewa heshima (‘dulia’) na Bikira Maria heshima zaidi (‘yuper-dulia’).
Kanisa Katoliki linakiri neema zote za Mungu zinampitia Maria.
BIKIRA MARIA KATI YA WAORTHODOKSI
Kwa kiasi
kikubwa imani ya Waorthodoksi kuhusu Maria inalingana na ile ya Wakatoliki,
ingawa hawakubali jinsi baadhi ya dogma hizo zilivyotangazwa na jinsi
zinavyofafanuliwa.
Martin Luther alipoanza Matengenezo ya Kiprotestanti aliandika kwa
heshima juu ya Bikira Maria, lakini kadiri mabishano yalivyozidi kati ya madhehebu ya Kikristo,
Waprotestanti walizidi kupinga mafundisho ya Kanisa Katoliki juu ya Mama wa
Yesu. Siku hizi baadhi yake, hasa Waanglikana na Wamethodisti wanamrudishia Maria nafasi yake kama
kielelezo cha imani na cha kupokea neema ya Mungu.
Kurani inamtaja
mwanamke mmoja tu, tena mara 34: ni Mariamu, mama wa nabii Isa. Akichanganywa
na dada wa Haruni na Musa,
aliyekuwa na jina hilohilo, anatajwa kama binti Imrani. Pia habari
nyingine kadhaa zinapishana na zile za Injili.
Hata hivyo
anapewa heshima ya pekee, kama inavyoonekana katika sura ya 3:43: “Na kumbukeni
malaika waliposema, ‘Ewe Mariamu, kwa hakika Mwenyezi Mungu amekuchagua na
kukutakasa na kukutukuza kuliko wanawake wa walimwengu”. Tena katika aya 3:46:
“Na kumbukeni waliposema malaika: ‘Ewe Mariamu, bila shaka Mwenyezi Mungu
anakupa habari njema za Neno litokalo kwake, jina lake Masihi Isa mwana wa
Mariamu, mwenye heshima katika dunia na ahera, na yu miongoni mwa
waliokaribishwa’”.
Aliambiwa
amefanywa “ishara” pamoja na mwanae, ingawa haisemwi ni ishara ya nini. Sura ya
19, yenye jina lake, inaeleza kwamba Malaika Jibrili (Gabrieli) akimpasha
habari ya mimba alisema, ‘Hakika mimi ni mjumbe wa Mola wako ili nikupe mwana
mtakatifu’. Akasema, ‘Ninawezaje kupata mtoto hali hajanigusa mwanamume yeyote,
wala mimi si mwasherati?’ Akasema, ‘Ni kama hivyo; Mola wako amesema: Haya ni
rahisi kwangu, na ili tukufanya ishara kwa mwanadamu na rehema itokayo kwetu,
na ni jambo lililokwisha hukumiwa’ ” (19:19-21). “Na mwanamke yule aliyejilinda
tupu yake na tukampulizia roho yetu na tukamfanya yeye na mwanawe ishara kwa
walimwengu” (21:91).
Pamoja na
kusifiwa kwa usafi wake, anaongezewa sifa za imani na unyenyekevu: “Na Mariamu
binti Imrani aliyejilinda uchi wake, na tukampulizia humo Roho yetu na
kayasadikisha maneno ya Mola wake, na vitabu vyake; na alikuwa miongoni mwa
wanyenyekevu” (66:12).
0 comments:
Post a Comment