MATANDA RICHARD ANAELIMISHA JAMII KWA MAHUBIRI YAKE.
Uso mwangavu kama jua "Aligeuka sura
yake mbele yao; uso wake ukang'aa kama jua" (Math 17:2). Ukurasa wa Injili
wa Kristo kugeuka sura, ambapo mitume watatu Petro, Yakobo na Yohane
wanaonekana kama wamechanganyikiwa na uzuri wa Mkombozi, unaweza kuchukuliwa
kama picha ya sala hasa ya Kikristo. Kuukazia macho uso wa Kristo, kutambua
fumbo lake katika safari ya kawaida na ya uchungu ya ubinadamu wake, hadi
kuhisi uangavu wa Kimungu uliodhihirika moja kwa moja katika Mfufuka
aliyetukuzwa kuumeni kwa Baba, ndiyo kazi ya kila mfuasi wa Kristo; kwa hiyo ni
kazi yetu pia. Tukiukazia macho uso huo tunajiweka tayari tuupokee fumbo la
uzima wa Utatu mtakatifu, ili kung'amua kwa namna mpya daima upendo wa Baba na
kujaa furaha ya Roho Mtakatifu. Hapo linatimia kwetu pia neno la mtume Paulo:
"Tukiurudisha utukufu wa Bwana, kama vile katika kioo, tunabadilishwa
tufanane na mfano uo huo, toka utukufu hata utukufu, kama vile kwa utukufu
utokao kwa Bwana, aliye Roho" (2Kor 3:18).
Maria kielelezo cha sala hasa
Maria ni kielelezo
bora cha kumkazia macho Kristo. Sura ya Mwana ni ya kwake kwa namna ya pekee.
Alitungwa tumboni mwake, akichukua toka kwake sura ya kufanana naye kibinadamu
ambayo inadokeza ujirani wa Kiroho ambao kwa hakika ni mkubwa zaidi. Hakuna
aliyejitolea kuukazia macho uso wa Kristo kuliko alivyofanya Maria. Kwa namna
fulani macho ya moyo wake yalianza kumuelekea tangu apashwe habari,
alipomchukua mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu; miezi iliyofuata alianza kuhisi
uwemo wake tumboni na kutabiri sura yake. Hatimaye alipomzaa Bethlehemu macho
ya mwili wake pia yaliuelekea kwa hisani uso wa Mwana, huku akimvika nguo za
kitoto na kumlaza horini (taz. Lk 2:7).
Tangu hapo mtazamo wake,
uliojaa daima mshangao wa kiibada, haukubandukana naye tena. Pengine ukawa
mtazamo wa kuuliza swali, kama vile katika tukio la Yesu kupotea hekaluni:
«Mwanangu, mbona umetutenda hivi?» (Lk 2:48); kwa vyovyote ukawa mtazamo wa
kupenya, unaoweza kusoma moyoni mwa Yesu, hata kuhisi miguso iliyofichika na
kutabiri machaguo yake, kama alivyofanya Kana (taz. Yoh 2:5); mara nyingine
ukawa mtazamo wenye uchungu, hasa chini ya msalaba ambapo ukawa tena, kwa namna
fulani, mtazamo wa 'mwanamke anayejifungua', kwa kuwa Maria hakushiriki tu
mateso na kifo cha Mwana pekee, bali alimpokea mtoto mpya aliyekabidhiwa katika
mwanafunzi mpendwa (taz. Yoh 19:26-27); asubuhi ya Pasaka ukawa mtazamo
mwangavu kwa furaha ya ufufuko na hatimaye ukawa mtazamo motomoto kwa ajili ya
Roho kumiminwa siku ya Pentekoste (taz. Mdo 1:14).
Kumbukumbu za Maria
Maria aliishi macho
kwa Kristo na kutia maanani kila neno lake: «Aliyaweka maneno hayo yote,
akiyafikiri moyoni mwake» (Lk 2:19; taz. 2:51). Kumbukumbu za Yesu,
zilizochapika rohoni mwake, zilimfuata katika nafasi yoyote, zikimfanya arudie
kimawazo matukio mbalimbali ya maisha yake karibu na Mwana. Kumbukumbu hizo
ndizo zilizounda, kwa namna fulani, 'rozari' ambayo mwenyewe alisali mfululizo
siku zote za maisha yake duniani.
Pia sasa, kati ya nyimbo
za furaha za Yerusalemu wa mbinguni, sababu zake za kushukuru na kusifu
zinabaki zilezile. Ndizo zinazomuelekeza kulishughulikia kimama Kanisa
linalohiji, ambapo mwenyewe anaendelea kutekeleza tangazo lake kama
mwenezainjili. Maria anawapendekezea mfululizo waamini 'mafumbo' ya Mwanae,
akitamani yatazamwe yaweze kueneza uwezo wote wa kuokoa uliyo nayo. Jumuia ya
Kikristo inaposali Rozari inajilinganisha na kumbukumbu na mtazamo wa Maria.
Rozari, sala ya kuzamia mafumbo ya imani
Rozari, kuanzia
mang'amuzi yenyewe ya Maria, ni sala hasa ya kuzamia mafumbo ya imani. Ingekosa
sura hiyo isingekuwa yenyewe tena, kama alivyosisitiza Paulo VI: «Pasipo kuzama
katika mafumbo, Rozari ni kama mwili usio na roho, na inaingia hatari ya
kukariri maneno kimashine tu na hivyo kupinga onyo la Yesu: 'Mkiwa katika kusali,
msipayukepayuke, kama watu wa mataifa; maana wao hudhani ya kuwa watasikiwa kwa
sababu ya maneno yao kuwa mengi' (Math. 6:7). Kwa maumbile yake, sala ya Rozari
inadai mwendo mtulivu na kama kusimama kwa kuwaza, ambavyo vimsaidie anayesali
atafakari mafumbo ya maisha ya Bwana, ambayo yatazamwe kupitia moyo wa Mama
yule aliyekuwa karibu zaidi na Bwana, na vifunue utajiri wake usiopimika».
Inafaa tuzingatie wazo
hilo la dhati la Paulo VI, ili kutokeza sura mbalimbali za Rozari ambazo
zinatia maanani sifa yake ya kuwa sala ya kumkazia macho Kristo.
Kumkumbuka Kristo pamoja na Maria
Kwa Maria, kuzama
katika mafumbo ni hasa kukumbuka. Lakini ni lazima tuelewe hilo kwa maana ya
Kibiblia ya neno (zakar), ambayo inafanya matendo aliyoyatenda Mungu katika
historia ya wokovu yawe ya leo. Biblia ni simulizi la matukio ya wokovu, ambayo
kilele chake ni Kristo mwenyewe. Matukio hayo siyo "jana" tu, bali ni
"leo" ya wokovu. Jambo hilo la kufanya tukio lililopita liwe la leo
pia linatendeka hasa katika liturujia: yale ambayo Mungu aliyatenda karne
kadhaa zilizopita hayawahusu tu wale walioyashuhudia kwa wakati wake, bali
yanamfikia kwa zawadi yake ya neema mtu wa wakati wowote. Kwa namna fulani hilo
ni kweli pia kwa njia nyingine za kujihusisha kwa imani na matukio hayo:
«kuyakumbuka» kwa msimamo wa imani na upendo, maana yake ni kujiweka wazi
kupokea neema ambayo Kristo ametupatia kwa mafumbo ya maisha, kifo na ufufuko
wake.
Kwa hiyo, wakati ni
lazima tusisitize tena pamoja na Mtaguso wa pili wa Vatikano kwamba liturujia,
iliyo utekelezaji wa ukuhani wa Kristo na ibada rasmi ya hadhara, ndiyo «kilele
ambacho utendaji wote wa Kanisa unakilenga na papo hapo chemchemi ambamo nguvu
zake zote zinabubujika», ni lazima pia tukumbuke kwamba maisha ya Kiroho
«hayaishii katika kushiriki liturujia takatifu tu. Mkristo ameitwa kusali
pamoja na wenzake, hata hivyo anatakiwa pia kuingia katika chumba chake cha
ndani ili kumuomba Baba sirini (taz. Mt 6:6); tena anatakiwa kusali bila ya
kikomo, kama mtume Paulo alivyofundisha (taz. 1Ts 5:17)». Rozari inaingia kwa
namna yake maalumu katika mandhari hiyo
yote ya sala 'isiyokoma', na ikiwa liturujia, iliyo kazi ya Kristo na ya Kanisa
lake, ni kazi ya wokovu kwa namna bora, Rozari, iliyo tafakuri juu ya Kristo
pamoja na Maria, ni kuzama ndani ya mafumbo kunakoleta wokovu. Kwa kuwa kuzama
katika maisha ya Mkombozi, fumbo baada ya fumbo, kunasababisha kwamba, yale
ambayo mwenyewe aliyatenda na ambayo liturujia inafanya yawe ya leo, yapokewe
na mwamini kwa dhati na kuunda maisha yake.
Kufundishwa na Maria juu ya Kristo
Kristo ndiye Mwalimu
hasa, yeye aliye mfunuaji na ufunuo wenyewe. Si swala la kujifunza tu maneno
aliyoyafundisha, bali la 'kumsoma mwenyewe'. Lakini nani mwalimu mzoefu kuliko
Maria katika jambo hilo? Ikiwa upande wa Mungu Roho Mtakatifu ndiye Mwalimu wa
ndani anayetufikisha kwenye ukweli wote wa Kristo (taz. Yoh 14:26; 15:26;
16:13), upande wa binadamu hakuna anayemfahamu Kristo vizuri kuliko Maria,
hakuna anayeweza kama Mama yake kutuingiza katika ujuzi wa dhati wa fumbo lake.
'Ishara'
ya kwanza iliyotendwa na Yesu - kugeuza maji kuwa divai kwenye arusi ya Kana -
inatuonyesha Maria katika nafasi hiyo ya mwalimu, akiwahimiza watumishi
watekeleze maagizo ya Kristo (taz. Yoh 2:5). Na tunaweza kubuni kwa hakika
kwamba, kazi hiyo mwenyewe aliifanya kwa ajili ya wanafunzi baada ya Yesu kupaa
mbinguni, ambao alibaki pamoja nao wakimngojea Roho Mtakatifu, akawafariji
katika mwanzo wa utume wao. Kupitia pamoja na Maria mafumbo ya Rozari ni kama
kuketi 'shuleni' pa Maria ili kumsoma Kristo, ili kupenya siri zake, ili
kuelewa ujumbe wake. Shule hiyo ya Maria inaleta faida kubwa, hasa tukizingatia
kwamba anafanya kazi hiyo kwa kutupatia kwa wingi vipaji vya Roho Mtakatifu na
papo hapo kwa kutupendekezea mfano wa ile «hija ya imani», ambayo yeye ni
mwalimu wake asiye na kifani. Mbele ya kila fumbo la Mwanae, mwenyewe
anatualika, kama alivyofanya siku aliyopashwa habari na malaika, tuulize kwa
unyenyekevu maswali yanayotufungulia mwanga, halafu tumalizie daima kwa utiifu
wa imani: «Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema» (Lk
1:38).
Kujilinganisha na Kristo pamoja na Maria
Maisha ya Kiroho ya
Kikristo sifa yake kuu ni juhudi ya mwanafunzi kujilinganisha na Mwalimu wake
zaidi na zaidi (taz. Rom 8:29; Fil 3:10,21). Miminiko la Roho katika ubatizo,
linalomwingiza mwamini kama tawi ndani ya mzabibu ambao ni Kristo (taz. Yoh 15:5),
linamfanya kiungo cha mwili wake wa fumbo (taz. 1Kor 12:12; Rom 12:5). Lakini
umoja huo wa msingi unatakiwa kufuatwa na safari ya kuungana naye zaidi na
zaidi, ambayo ielekeze zaidi na zaidi mwenendo wa mwanafunzi kadiri ya 'nia' ya
Kristo: «Iweni na nia iyohiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo
Yesu » (Fil 2:5). Kadiri ya maneno ya Mtume ni lazima «kumvaa Kristo» (taz. Rom
13:14; Gal 3:27).
Katika safari ya Kiroho
ya Rozari, ambayo msingi wake ni kuukazia macho mfululizo uso wa Kristo pamoja
na Maria, kipeo hicho kigumu cha kujilinganisha naye kinalengwa kwa njia ya
kumkaribia 'kirafiki'. Hiyo inatuingiza kwa urahisi katika maisha ya Kristo na
kutufanya 'tupumue' hisia zake. Kuhusu jambo hilo mwenye heri Bartolo Longo
alisema, «Kama vile marafiki wawili, wakishirikiana mara nyingi, huwa
wanafanana katika mwenendo pia, sisi tukiongea kidugu na Yesu na Bikira, katika
kutafakari mafumbo ya Rozari, na kuishi pamoja nao kwa Ekaristi, tunaweza
kufanana nao, kadiri unyonge wetu unavyoruhusu, na kujifunza kutoka kwa
vielelezo hivyo bora maisha ya unyenyekevu, ya ufukara, yaliyofichika, ya
subira na makamilifu».
Kwa safari hiyo ya
kujilinganisha na Kristo, katika Rozari tunajiaminisha kwa namna ya pekee kwa
kazi ya kimama ya Bikira mtakatifu. Yeye aliye mzazi wa Kristo, huku akiwa mwenyewe kiungo cha Kanisa, tena «kiungo bora
na cha pekee kabisa», kwa wakati huohuo ni pia 'Mama wa Kanisa'. Kulingana na
hadhi hiyo anazidi 'kuzaa' wana kwa Mwili wa fumbo wa Mwanae. Anafanya hivyo
kwa njia ya dua, akiwaombea miminiko la Roho ambalo halina mwisho. Maria ndiye
picha kamili ya umama wa Kanisa.
Rozari inatusogeza
kifumbo karibu na Maria aliyewajibika kusaidia ustawi wa kibinadamu wa Kristo
katika nyumba ya Nazareti. Hiyo inamwezesha kutulea na kutuunda kwa juhudi
hizohizo hadi Kristo “aundwe” kikamilifu ndani mwetu (taz. Gal 4:19). Kazi hiyo
ya Maria, ambayo inategemea na kulenga kabisa ile ya Kristo, “haizuii hata
kidogo muungano wa moja kwa moja wa waamini na Kristo, bali inausaidia”. Ndilo
wazo angavu lililotokezwa na Mtaguso wa pili wa Vatikano, ambalo nimeling'amua
kwa nguvu sana maishani mwangu, nikilifanya msingi wa tamko langu la kiaskofu: Totus tuus. Inavyoeleweka, tamko hilo
linatokana na mafundisho ya mtakatifu Alois Maria Grignion de Montfort, ambaye
alieleza ifuatavyo nafasi ya Maria katika safari ya kila mmojawetu ya
kujilinganisha na Kristo: «Ukamilifu wetu wote umo katika kulingana, kuungana
na kuwekwa wakfu kwa Yesu Kristo. Kwa hiyo bila ya shaka ibada iliyo kamili
kuliko zote ni ile ambayo inatulinganisha, inatuunganisha na kutuweka wakfu
kikamilifu zaidi kwa Yesu Kristo. Basi, kwa kuwa Maria ndiye kiumbe
aliyelingana zaidi na Yesu Kristo, kati ya ibada zote ile inayomweka wakfu na
kumlinganisha zaidi mtu kwa Bwana wetu ni ibada kwa Maria, Mama yake mtakatifu,
tena kadiri atakavyowekwa wakfu kwake atawekwa wakfu kwa Yesu Kristo». Hakuna
nafasi nyingine kuliko Rozari ambapo njia ya Kristo na ya Maria zinaonekana
kuwa ni moja kwa dhati. Maria anaishi ndani ya Kristo tu na kwa ajili ya Kristo!
Kumuomba Kristo pamoja na Maria
Kristo ametualika
tumuelekee Mungu kwa udumifu na tumaini ili tusikilizwe: «Ombeni, nanyi
mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa» (Math 7:7).
Msingi wa uwezo huo wa sala ni wema wa Baba, lakini pia ushenga wa Kristo
mwenyewe mbele yake (taz. 1Yoh 2:1) na kazi ya Roho Mtakatifu ambaye
«hutuombea» kadiri ya mipango ya Mungu (taz. Rom 8:26-27). «Kwa maana hatujui
kuomba jinsi itupasavyo» (Rom 8:26) na pengine hatusikilizwi kwa sababu
«tunaomba vibaya» (taz. Yak 4:2-3).
Ili kuchangia sala
ambayo Kristo na Roho wanabubujisha moyoni mwetu, Maria anaingia kati kwa
maombezi yake ya kimama. «Sala ya Kanisa ni kama inategemezwa na sala ya
Maria». Kwa kweli, Yesu, mshenga pekee, akiwa ndiye njia ya sala yetu, Maria,
aliye picha yake angavu, anaionyesha hiyo njia na «kwa msingi wa ushirikiano
huo wa pekee wa Maria na kazi ya Roho Mtakatifu, Makanisa yamestawisha sala kwa
Mama mtakatifu wa Mungu, yakifanya ilenge kwenye nafsi ya Kristo
iliyodhihirishwa katika mafumbo yake». Kwenye arusi ya Kana Injili inaonyesha
hiyo nguvu ya maombezi ya Maria, aliyejifanya sauti ya shida za watu kwa Yesu:
«Hawana divai» (Yoh 2:3).
Rozari ni tafakuri na
dua kwa pamoja. Kumlilia kwa bidii Mama wa Mungu, msingi wake ni tumaini la
kwamba maombezi yake ya kimama yanaweza yote moyoni mwa Mwanae. Alivyosema
mwenye heri Bartolo Longo katika Dua kwa Bikira, akitumia neno la kusisimua
linalohitaji kueleweka vizuri, Maria ni «Mwenyezi kwa neema». Hakika hiyo,
ambayo chanzo chake ni Injili, imeimarishwa na mang'amuzi ya taifa la Kristo.
Mwanashairi bora Dante aliitafsiri vizuri ajabu, kufuatana na mtakatifu Bernardo, akiimba: «Mama, wewe u mkuu na
mwenye uwezo hivi kwamba, / anayetaka
neema asikukimbilie wewe, / hamu yake inataka kuruka pasipo mabawa». Maria,
patakatifu pa Roho Mtakatifu (taz. Lk 1:35), wakati anapoombwa nasi katika
Rozari, anatusimamia mbele ya Baba aliyemjaza neema na ya Mwana aliyezaliwa
kutoka tumboni mwake, akisali pamoja nasi na kwa ajili yetu.
Kumtangaza
Kristo pamoja na Maria
Rozari ni pia safari
ya kutangaza na kuchimba, ambamo fumbo la Kristo linatokezwa upya mfululizo kwa
ngazi mbalimbali za maisha ya Kikristo. Namna yake ni ya kulitokeza upande wa
sala na wa kuzama ndani ya mafumbo, ambayo inalenga kumuunda mfuasi kadiri ya
moyo wa Kristo. Kwa kweli katika kusali Rozari, ikiwa sehemu zake zote
zinazoweza kuchangia tafakuri ya nguvu zinatumika ipasavyo, inapatikana nafasi
muhimu ya katekesi, hasa katika adhimisho la kijumuia kwenye parokia na patakatifu.
Wachungaji wanatakiwa kuitumia nafasi hiyo. Bikira wa Rozari anaendelea hivyo
pia kazi yake ya kumtangaza Kristo. Historia ya Rozari inaonyesha jinsi sala
hiyo ilivyotumiwa hasa na Wadominiko, katika kipindi kilichokuwa kigumu kwa
Kanisa kutokana na uenezi wa uzushi. Leo tuko mbele ya changamoto mpya. Kwa
nini tusishike tena tasbihi mikononi kwa imani ile waliyokuwa nayo
waliotutangulia? Rozari inadumu kuwa na nguvu zake zote na kuendelea kuwa
silaha muhimu kati ya vifaa vya kichungaji vya kila mwenezainjili halisi.
SURA YA PILI
MAFUMBO
YA KRISTO - MAFUMBO YA MAMA
Rozari «muhtasari wa Injili»
Hatuwezi kuanza
kuukazia macho uso wa Kristo bila ya kusikiliza, katika Roho, sauti ya Baba,
kwa sababu «hakuna amjuaye Mwana, ila Baba» (Math 11:27). Karibu na Kaisarea
Filipi, baada ya ungamo la Petro, Yesu alifafanua asili ya hisi hiyo sahihi
hivi ya undani wake mwenyewe: «Mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba
yangu aliye mbinguni» (Math 16:17). Kwa hiyo ni lazima kufunuliwa kutoka juu.
Lakini ili tuupokee ufunuo huo ni lazima kusikiliza. Mang'amuzi ya kimya na ya
sala tu yanatupatia upeo wa kufaa ambapo unaweza kukomaa na kustawi ujuzi
halisi zaidi wa fumbo hilo, ambao unaunganisha na kutia uaminifu.
Rozari ni njia mojawapo
ya mapokeo ya sala ya Kikristo kwa ajili ya kuzama katika uso wa Kristo. Papa
Paulo VI aliifafanua hivi: « Rozari ikiwa sala ya Kiinjili, ambayo kiini chake
ni fumbo la umwilisho ulioleta ukombozi, basi ni sala inayomlenga Kristo moja
kwa moja. Kwa kuwa hata jambo lake maalumu zaidi - yaani kukariri kilitania Salamu Maria -
linakuwa sifa isiyokoma kwa Kristo, lengo kuu la tangazo la malaika na la
salamu ya mama wa Mbatizaji: 'Mzao wa tumbo lako amebarikiwa' (Lk 1:42). Tuseme
zaidi: kukariri Salamu Maria ni kama kitambaa ambacho juu yake tunafuma tendo
la kuzama katika mafumbo: Yesu anayekumbushwa na kila Salamu Maria ni yuleyule
ambaye mfululizo wa mafumbo unatutolea mara kwa mara kama Mwana wa Mungu na wa
Bikira».
Ukamilisho wa kufaa
Kati ya mafumbo
mengi ya maisha ya Kristo, Rozari, kwa jinsi ilivyoundika katika desturi
iliyopitishwa na mamlaka ya Kanisa, inayapendekeza machache tu. Chaguo hilo
lililazimishwa na mpango asili wa sala hiyo wa kulingana na idadi ya Zaburi
150.
Hata hivyo naona kwamba,
ili kuongeza uzito wa Kikristo wa Rozari, inafaa kuikamilisha kwa namna ambayo,
ingawa inaachwa ifanyiwe kazi kwa hiari na mtu mmojammoja na jumuia nzima,
iiwezeshe kukumbatia pia matendo ya maisha ya hadhara ya Kristo kati ya ubatizo
na mateso. Kwa kuwa katikati ya mafumbo hayo tunakazia macho pande muhimu za
nafsi ya Kristo kama yule aliyetufunulia Mungu moja kwa moja. Ndiye yule
ambaye, kisha kutambulishwa kama Mwana mpendwa wa Baba kwenye ubatizo katika
mto Yordani, aliutangaza ujio wa Ufalme, aliushuhudia kwa matendo na kutangaza
madai yake. Ni katika miaka ya maisha ya hadhara kwamba fumbo la Kristo lilidhihirika kwa namna ya
pekee kama fumbo la mwanga: «Muda nilipo ulimwenguni, mimi ni nuru ya
ulimwengu» (Yoh 9:5).
Basi, ili Rozari iweze
kuitwa kwa haki zaidi 'muhtasari wa Injili', inafaa kwamba, kisha kukumbuka
umwilisho na maisha yaliyofichika ya Kristo (mafumbo ya furaha), na kabla ya
kuzingatia uchungu wa mateso (mafumbo ya uchungu) na ushindi wa ufufuko
(mafumbo ya utukufu), tafakuri ilenge pia nafasi kadhaa za maana zaidi za
maisha ya hadhara (mafumbo ya mwanga). Ongezeko hilo la mafumbo mapya, bila ya
kuhatarisha jambo lolote la msingi katika sura ya kimapokeo ya sala hiyo,
linakusudiwa kuifanya izingatiwe upya katika maisha ya Kiroho ya Wakristo, kama
namna halisi ya kuingizwa vilindini mwa moyo wa Kristo, ulio kina kirefu cha
furaha na mwanga, uchungu na utukufu.
Mafumbo
ya furaha
Mfululizo wa kwanza,
ule wa 'mafumbo ya furaha', kwa kweli
sifa yake maalumu ndiyo furaha iliyosambazwa na tukio la umwilisho. Hiyo
ni wazi tangu Kupasha Habari, ambapo salamu ya Gabrieli kwa Bikira wa Nazareti inajilinganisha
na mwaliko wa kuwa na furaha ya Kimasiha: «Furahi, Maria». Tangazo hilo ni
lengo la historia yote ya wokovu, tena la historia ya ulimwengu pia. Kwa
sababu, ikiwa mpango wa Baba ni kujumlisha vyote katika Kristo (taz. Ef 1:10),
kwa namna fulani ulimwengu wote ndio uliofikiwa na fadhili ya Kimungu ambayo
Baba alimuinamia Maria ili kumfanya Mama wa Mwanae. Upande mwingine, binadamu
wote ni kama wanaingia ndani ya fiat
ambayo Maria aliyakubali mara matakwa ya Mungu.
Halafu
tukio la kukutana na Elizabeti limejaa shangwe, ambapo sauti yenyewe ya Maria
na uwemo wa Kristo tumboni mwake vilifanya Yohane «kikaruka kwa shangwe» (taz.
Lk 1:44). Limejaa furaha vilevile tukio la Bethlehemu, ambapo kuzaliwa kwa
Mtoto wa Kimungu, Mwokozi wa dunia, kuliimbwa na malaika na kutangazwa kwa
wachungaji kama «furaha kuu» (Lk 2:10).
Lakini mafumbo mawili ya
mwisho, ingawa yanaendelea kuwa na ladha ya furaha, yanadokeza tayari dalili za
janga. Kwa kuwa Kutolewa hekaluni, huku kukitokeza furaha ya kuwekwa wakfu na
ya kumzamisha mzee Simeoni katika fumbo, kunaleta pia utabiri juu ya «ishara
itakayonenewa» ambayo huyo Mtoto atakuwa kwa Israeli, na juu ya upanga
utakaochoma moyo wa Mama (taz. Lk 2:34-35). Vilevile ni la furaha na la
kusikitisha kwa pamoja tukio la Yesu hekaluni akiwa na umri wa miaka kumi na miwili.
Hapo alitokea katika hekima yake ya Kimungu, huku akisikiliza na kuhoji, akiwa
kimsingi yule mwenye 'kufundisha'. Ufunuo wa fumbo lake kama Mwana
anayewajibika kabisa kwa mambo ya Baba ni tangazo la ile nia imara ya Kiinjili
ambayo mbele ya madai ya moja kwa moja ya Ufalme inatia shakani hata
mafungamano mapendevu zaidi kwa binadamu. Yosefu na Maria wenyewe,
waliohangaika na kufadhaika, «hawakuelewa na neno hilo alilowaambia» (Lk 2:50).
Hivyo kutafakari mafumbo
'ya furaha' ni kuingia ndani ya sababu kuu na maana ya dhati ya furaha ya
Kikristo. Ni kukazia macho uhalisi wa fumbo la umwilisho na utabiri usio wazi
wa fumbo la uchungu wenye kuokoa. Maria anatuongoza tuelewe siri ya furaha ya
Kikristo, akitukumbusha kwamba Ukristo ni hasa euangelion, 'habari njema', ambayo kiini chake, tena yaliyomo yake
yote ni nafsi ya Kristo, Neno aliyefanyika mwili, Mwokozi pekee wa ulimwengu.
Mafumbo ya mwanga
Sala hasa, ikivuka
toka utoto na maisha ya Nazareti hadi maisha ya hadhara ya Yesu, inatufikisha
kwenye mafumbo ambayo yanaweza kuitwa kwa namna ya pekee 'mafumbo ya mwanga'.
Kwa kweli, fumbo lote la Kristo ni mwanga. Ndiye «nuru ya ulimwengu» (Yoh
8:12). Lakini sifa hiyo inajitokeza hasa katika miaka ya maisha ya hadhara,
ambapo yeye alitangaza habari njema ya Ufalme. Nikitaka kuionyesha jumuia ya
Kikristo nafasi tano za maana - mafumbo 'ya mwanga' – za kipindi hicho cha
maisha ya Kristo, naona inafaa kuzibainisha kama ifuatavyo: 1. katika ubatizo
wake kwenye Yordani, 2. katika kujifunua kwake kwenye arusi ya Kana, 3. katika
kutangaza Ufalme wa Mungu pamoja na mwaliko wa kuongoka, 4. katika kung’aa
kwake alipogeuka sura, na, hatimaye, 5. katika kuweka ekaristi, sakramenti ya
fumbo la Pasaka.
Kati ya mafumbo hayo
kila mojawapo linafunua Ufalme uliokwishafika katika nafsi yenyewe ya Yesu.
Kwanza, ubatizo kwenye Yordani. Hapo, Kristo aliposhukia maji ya mto, kama yule
asiye na doa anayejifanya ‘dhambi’ kwa ajili yetu (taz. 2Kor 5:21), mbingu zilifunguka
na sauti ya Baba ilimtangaza kuwa ni Mwanae mpenzi (taz. Math 3:17 na aya
sambamba), huku Roho akimshukia ili kumweka wakfu kwa utume unaomkabili. Pili,
mwanzo wa ishara huko Kana (taz. Yoh 2:1-12), ambapo Kristo, akigeuza maji kuwa
divai, aliifungua mioyo ya wanafunzi isadiki kutokana na Maria kuingilia kati,
yeye aliye wa kwanza kati ya waamini. Tatu, mahubiri ambayo Yesu alitangaza
ujio wa Ufalme wa Mungu na kualika watu watubu (taz. Mk 1:15), akiondolea
dhambi za wanaomkaribia kwa tumaini nyenyekevu (taz. Mk 2:3-13; Lk 7:47-48),
mwanzo wa ile huduma ya huruma atakayoendelea kutoa hadi mwisho wa dunia, hasa
kwa njia ya sakramenti ya upatanisho aliyolikabidhi Kanisa lake (taz. Yoh
20:22-23). Halafu kwa namna ya pekee tukio la kugeuka sura, ambalo kadiri ya
mapokeo lilitokea juu ya mlima Tabori. Utukufu wa umungu uling’aa katika uso wa
Kristo, huku Baba akimtambulisha kwa mitume waliochanganyikiwa na uzuri huo
akidai wamsikilize (taz. Lk 9:35 na aya sambamba) na wajiandae kuishi pamoja
naye nafasi chungu ya mateso, ili kufikia pamoja naye furaha ya ufufuko na
maisha yaliyogeuzwa sura na Roho Mtakatifu. Hatimaye, ni fumbo la mwanga tendo
la kuweka ekaristi, ambamo Kristo anajifanya chakula kwa Mwili wake na Damu
yake ndani ya maumbo ya mkate na divai, akishuhudia «upeo» wa upendo wake kwa
ajili ya ulimwengu (Yoh 13:1), ambao akajitoa sadaka kwa wokovu wake.
Uwepo wa Maria
hauonekani katika mafumbo hayo, isipokuwa Kana. Injili zinadokeza tu mara moja
moja uwepo wake katika nafasi hii au hii ya mahubiri ya Yesu (taz. Mk 3:31-35;
Yoh 2:12) na hazisemi kitu kuhusu uwezekano wa kuwepo kwake karamuni wakati wa
kuweka ekaristi. Lakini kazi aliyoifanya Kana inasindikiza, kwa namna fulani,
safari yote ya Kristo. Ufunuo ule ambao katika ubatizo kwenye Yordani ulitolewa
na Baba moja kwa moja ukarudiwa na Mbatizaji kama mwangwi wake, huko Kana
ulikuwemo kinywani mwa Maria, ulipogeuka kuwa onyo kuu la kimama ambalo
analitoa kwa Kanisa la nyakati zote: «Lolote atakalowaambia, fanyeni» (Yoh
2:5). Hilo ni onyo linalofaa kutangulia maneno na ishara ya Kristo katika
maisha ya hadhara, likiendelea kuonekana nyuma ya 'mafumbo yote ya mwanga' ili
tuyazingatie kadiri ya Maria.
Mafumbo ya uchungu
Katika kudhalilishwa
hivyo haufunuliwi tu upendo wa Mungu, bali pia maana yenyewe ya binadamu. Ecce homo: anayetaka kufahamu mtu
alivyo, anapaswa kutambua maana, mzizi na utimilifu wake katika Kristo, Mungu
aliyejishusha kwa upendo «hata mauti, naam, mauti ya msalaba» (Fil 2:8).
Mafumbo ya uchungu yanamuongoza mwamini kuishi upya kifo cha Yesu kwa kujiweka
chini ya msalaba karibu na Maria, ili kuzama pamoja na Mama katika kilindi cha
upendo wa Mungu kwa binadamu na kuhisi nguvu zake zote za kuletea uhai mpya.
Mafumbo ya utukufu
«Kuukazia macho uso
wa Kristo hakuwezi kuishia kwenye picha yake kama msulubiwa. Yeye yupo
amefufuka!». Tangu zamani Rozari inatokeza hakika hiyo ya imani, ikimualika
mwamini avuke ng’ambo ya giza la mateso, ili kuukazia macho utukufu wa Kristo
katika ufufuko na katika Kupaa mbinguni. Mkristo akimkazia macho Mfufuka
anavumbua upya sababu za imani yake (taz. 1Kor 15:14), na kuishi upya furaha
sio tu ya wale ambao Kristo aliwatokea – mitume, Magdalena, wanafunzi wa Emau
-, bali pia furaha ya Maria, ambaye alitakiwa kuwa na mang’amuzi si mapungufu
ya uhai mpya wa Mwana aliyetukuzwa. Katika utukufu huo ambao, kwa Kupaa kwake,
ulimweka Kristo kuumeni kwa Baba, Maria mwenyewe akainuliwa kwa Kupalizwa
kwake, akifikia, kwa fadhili ya pekee kabisa, kutanguliza hali waliyoandaliwa waadilifu
wote kwa ufufuko wa mwili. Hatimaye, akitiwa taji la utukufu – anavyoonekana
katika fumbo la mwisho la utukufu – anang’aa kama Malkia wa malaika na wa
watakatifu, utangulizi na kilele cha hali ya milele ya Kanisa.
Kama kiini cha safari
hiyo ya utukufu wa Mwana na wa Mama, Rozari inaipanga, katika fumbo la tatu la
utukufu, Pentekoste, inayoonyesha uso wa Kanisa kama familia iliyounganika na
Maria, iliyouhishwa na miminiko la nguvu la Roho, iliyo tayari kwa utume wa
uinjilishaji. Kuzama katika fumbo hilo, sawa na mafumbo mengine ya utukufu,
kunatakiwa kuwafanya waamini waelewe kwa namna hai zaidi na zaidi maisha yao
mapya katika Kristo, ndani ya ukweli wa Kanisa, maisha ambayo tukio la
Pentekoste ndiyo ‘picha' yake bora. Hivyo mafumbo ya utukufu yanalisha ndani ya
waamini tumaini la lengo la milele wanalolielekea kama viungo vya taifa la
Mungu linalohiji katika historia. Hiyo inatakiwa kuwasukuma washuhudie kishujaa
ile «habari njema» inayotia maanani maisha yao yote.
Toka 'mafumbo' hadi 'fumbo': njia ya Maria
Rozari inataka kutumikia
kipeo hicho, ikitolea 'siri' ya kujiweka wazi kwa urahisi zaidi kumjua Kristo
kwa dhati na kwa kuwajibika zaidi. Tunaweza kuiita njia ya Maria. Ni njia ya
kielelezo cha Bikira wa Nazareti, mwanamke wa imani, wa kimya na wa usikivu. Ni
pia njia ya ibada ya Kimaria inayohuishwa na hakika ya fungamano la moja kwa
moja kati ya Kristo na Mama yake mtakatifu sana: kwa namna fulani, mafumbo ya
Kristo ni pia mafumbo ya Mama, hata pale asipohusika moja kwa moja, kutokana na
kwamba Maria aliishi ndani ya Yesu na kwa ajili yake. Katika Salamu Maria
tukijitwalia maneno ya malaika Gabrieli na ya mtakatifu Elizabeti, tunajisikia
msukumo wa kumtafuta upya daima kwa Maria, katika mikono yake na katika moyo
wake, yule «mzao wa tumbo lake aliyebarikiwa» (taz. Lk 1:42).
Fumbo la Kristo, 'fumbo' la binadamu
Katika ushuhuda
niliokwishataja kwamba niliutoa mwaka 1978 kuwa Rozari ndiyo sala yangu pendevu
kuliko zote, nilitokeza wazo ambalo nataka kulisisitiza.
Hapo nilisema kuwa «sala
sahili ya Rozari inapiga madundo ya maisha ya binadamu». Kwa mwanga wa tafakuri
za hapa juu kuhusu mafumbo ya Kristo, si vigumu kuchimba uhusiano huo wa Rozari
na ubinadamu. Uhusiano huo ni wa msingi kuliko unavyoonekana mara moja.
Anayetulia katika kumkazia macho Kristo kwa kufuata hatua za maisha yake,
hawezi kukosa kukuta ndani mwake ukweli kuhusu binadamu pia. Ndio tamko kuu la
Mtaguso wa pili wa Vatikano, ambalo nimelifundisha mara nyingi kuanzia barua
rasmi Redemptor Hominis: «Kwa kweli,
fumbo la binadamu linaeleweka vizuri katika fumbo la Neno aliyefanyika mwili
tu». Rozari inasaidia kujiandaa kupokea mwanga huo. Kwa kufuata safari ya Kristo,
ambamo safari ya binadamu «imejumlishwa», imefunuliwa na kukombolewa, mwamini
anajiweka mbele ya sura ya mtu halisi. Akikazia macho kuzaliwa kwake anajifunza
uhai ulivyo mtakatifu, akitazama nyumba ya Nazareti anajifunza ukweli asili
kuhusu familia kadiri ya mpango wa Mungu, akimsikiliza Mwalimu katika mafumbo
ya maisha ya hadhara anapokea mwanga ili kuingia katika Ufalme wa Mungu na,
akimfuata katika njia ya Kalivari, anajifunza maana ya uchungu kwa wokovu.
Hatimaye, akiwakazia macho Kristo na Mama yake katika utukufu, anaona lengo
ambalo kila mmoja ameitiwa, akikubali kuponywa na kugeuzwa sura na Roho
Mtakatifu. Hivyo tunaweza kusema kuhusu kila fumbo la Rozari kwamba,
likizingatiwa vizuri, linaangaza fumbo la binadamu.
Wakati huohuo, inamtokea
mtu, hata bila ya kukusudia, kuleta kwenye mkutano huo na utu mtakatifu wa
Mkombozi matatizo, mafadhaiko, kazi na mipango mingi ambayo inaathiri maisha
yetu. «Umtwike Bwana mzigo wako naye atakutegemeza » (Zab 56:22). Kutafakari
kwa njia ya Rozari ni kukabidhi mahangaiko yetu kwa mioyo yenye huruma ya
Kristo na Mama yake. Miaka ishirini na tano baadaye, nikikumbuka majaribu
ambayo sijayakosa katika kutimiza huduma ya Petro, najisikia kusisitiza, kama
mwaliko wa dhati kwa wote wa kujipatia mang’amuzi hayo, kwamba kweli Rozari
«inapiga madundo ya maisha ya binadamu», ili yalingane na madundo ya maisha ya
Mungu, katika ushirika mfurahivu na Utatu mtakatifu, lengo na shauku ya maisha
yetu.
SURA YA TATU
KWANGU
MIMI KUISHI NI KRISTO
Rozari, njia ya kulishiza fumbo
Kutafakari mafumbo
ya Kristo kunapendekezwa katika Rozari kwa mbinu maalumu, ambayo kwa maumbile
yake inafaa kusaidia kuyalishiza. Ni mbinu ambayo msingi wake ni kukariri. Hiyo
ni kweli kwanza kwa Salamu Maria, inayorudiwa mara kumi kwa kila fumbo.
Tukitazama kijujuu tendo hilo la kukariri, tunaweza tukashawishika kuona Rozari
ni kazi kavu na ya kukinaisha. Kumbe inawezekana kuitathmini tasbihi tofauti
sana tukiiona kama tokeo la upendo usiochoka kumrudia mpenzi kwa maneno mengi
yaliyojaa hisia ambayo, ingawa yanaonekana kufanana, ni mapya daima kutokana na
hizo hisia unaoyajaa.
Katika Kristo, Mungu
ametwaa kweli «moyo wa nyama». Yeye hana tu moyo wa Kimungu, uliojaa huruma na
msamaha, bali pia moyo wa kibinadamu, unaoweza kupata mitikisiko yote ya
mapendo. Tungehitaji ushuhuda wa Injili kuhusu jambo hilo, isingekuwa vigumu
kuukuta katika majibizano ya kugusa kati ya Kristo na Petro baada ya ufufuko:
«Je, Simoni wa Yohane, wewe wanipenda?». Swali hilo liliulizwa hata mara tatu,
na jibu vilevile lilitolewa hata mara tatu: «Naam, Bwana, wewe wajua kuwa
nakupenda» (taz. Yoh 21:15-17). Mbali ya maana maalumu ya ukurasa huo, ulio
muhimu sana kwa utume wa Petro, hakuna anayekosa kuona uzuri wa kuyarudia hayo
mara tatu, ambapo sisitizo la swali na la jibu lake linajitokeza kwa maneno
yanayojulikana sana na mang’amuzi ya daima ya upendo wa binadamu. Ili tuielewe
Rozari, ni lazima tuingie katika mwendo wa saikolojia maalumu ya upendo.
Jambo moja ni wazi:
ikiwa marudio ya Salamu Maria yanamlenga moja kwa moja Maria, tendo la upendo
linamuendea hasa Yesu, pamoja na Maria na kwa njia yake. Marudio yanalishwa na
hamu ya kujilinganisha na Kristo kikamilifu zaidi na zaidi, ambako ndio
'mpango' halisi wa maisha ya Kikristo. Mtume Paolo alitamka mpango huo kwa
maneno ya moto: «Kwangu mimi kuishi ni Kristo, na kufa ni faida» (Fil 1:21).
Tena: «Ni hai; wala si mimi tena, bali Kristo yu hai ndani yangu» (Gal 2:20).
Rozari inatusaidia kukua katika kujilinganisha hivyo hadi lengo la utakatifu.
Mbinu
ya kufaa...
Si ajabu kwamba
fungamano na Kristo liweze kufaidika na msaada wa mbinu fulani pia. Mungu
anajishirikisha kwa binadamu akiheshimu maumbile yetu na mwendo wa maisha.
Ndiyo sababu maisha ya Kiroho ya Kikristo, ingawa yanaweza yakafikia namna za
juu zaidi za kimya cha kuzama katika mafumbo, ambapo picha zote, maneno na
matendo yote yanaachwa nyuma kutokana na nguvu ya muungano usiosemekana wa mtu
na Mungu, hata hivyo kwa kawaida ni sifa yake kumhusisha mtu mzima katika
maumbile yake changamano ya roho na mwili na katika mafungamano yake na
wengine.
Hiyo inaonekana wazi
katika liturujia. Sakramenti na visakramenti vimeundwa na mfululizo wa vitendo
ambavyo vinahusisha pande mbalimbali za nafsi yetu. Hata sala isiyo ya
liturujia inatokeza haja hiyohiyo. Hiyo inathibitishwa na kwamba huko Mashariki
sala maalumu zaidi ya tafakuri ya Kikristo, ambayo kiini chake ni maneno:
«Yesu, Kristo, Mwana wa Mungu, Bwana, unihurumie mimi mkosefu», inaendana
kimapokeo na mwendo wa kupumua, ambao, wakati unaposaidia kudumu katika dua,
unahakikisha uzito kama wa kimwili kwa hamu ya kumfanya Kristo awe pumzi, roho
na 'yote' ya maisha.
...
ambayo hata hivyo inaweza kuboreshwa
28. Katika barua ya
kitume Novo Millennio Ineunte
nilikumbusha kwamba leo, huku Magharibi pia, inasikika haja mpya ya kutafakari,
ambako pengine katika dini nyingine kuna namna za kuvutia. Hawakosekani Wakristo ambao, kwa kutojua vya
kutosha mapokeo ya Kikristo ya kuzama katika mafumbo, wanakubali kushawishiwa na
mapendekezo hayo. Lakini mara nyingi hayo kwa ndani msingi wake ni mawazo
yasiyokubalika, hata kama yana mambo mazuri ambayo yanaweza yakapatana na
mang’amuzi ya Kikristo. Katika mang’amuzi ya dini hizo pia zinatumika sana
mbinu ambazo, zikilenga roho ijikusanye kwa dhati, zinahusisha nafsi na mwili,
zinakariri maneno na kutumia ishara. Rozari inajipanga katika fremu hiyo ya
kimataifa ya mang’amuzi ya kidini, lakini inajibainisha kwa sifa za pekee
zinazolingana na madai maalumu ya Ukristo.
Kwa kweli Rozari ni
mbinu tu mojawapo ya kuzama katika mafumbo. Ikiwa ni mbinu inatakiwa kutumika
kuhusiana na lengo, isigeuke yenyewe kuwa lengo. Hata hivyo, ikiwa ni tunda la
mang’amuzi ya karne kadhaa, mbinu yenyewe inatakiwa kuthaminiwa vya kutosha.
Upande wake yanasimama mang’amuzi ya watakatifu wengi. Lakini hayo hayamaanishi
kwamba haiwezi kuboreshwa. Ndipo unapolenga ukamilisho wa mifululizo ya mafumbo
kwa mfululizo mpya wa mysteria lucis,
pamoja na mashauri kadhaa kuhusu namna ya kusali ambayo nayapendekeza katika
barua hii. Kwa njia yake sitaki kuvuruga muundo wa sala hiyo ulioimarika sana,
bali kusaidia waamini kuuelewa upande wa ishara kulingana na mahitaji ya maisha
ya kila siku. Pasipo hilo hatari siyo tu kwamba Rozari itashindwa kuzaa matunda
ya Kiroho yanayotarajiwa, bali pia kwamba tasbihi inayotumika kwa kawaida
kuisalia itakuja kutazamwa kama aina ya hirizi au chombo cha kishirikina kwa
kupotosha kabisa maana yake na kazi yake.
Kutaja fumbo
Kutaja fumbo, na kwa
wakati huohuo afadhali kupata nafasi ya kukazia macho picha inayolionyesha, ni
kama kuweka wazi mpangilio wa tukio la kulizingatia. Maneno yanaongoza ubunifu
na roho kwenye tukio maalumu au nafasi ya maisha ya Kristo. Katika maisha ya
Kiroho yaliyostawi ndani ya Kanisa, heshima kwa picha takatifu na vilevile
ibada mbalimbali zilizohusisha sana hizi za watu, tena na mbinu ile
iliyopendekezwa na mtakatifu Ignasi wa Loyola katika Mazoezi ya Kiroho,
zimetumia macho na ubunifu (compositio
loci), zikiviona kama msaada mkubwa kwa kukusanya roho katika fumbo. Tena
mbinu hiyo inalingana na mantiki yenyewe ya umwilisho: Mungu amependa kutwaa
katika Yesu sura ya binadamu. Ni kwa njia ya ukweli wa mwili wake kwamba sisi
tunaelekezwa kufungamana na fumbo lake la Kimungu.
Haja hiyo ya mambo ya
kushikika inaitikiwa pia na kule kutaja mafumbo mbalimbali ya Rozari. Bila ya
shaka hayo hayashiki nafasi ya Injili wala hayakumbushi kurasa zake zote. Kwa
hiyo Rozari haishiki nafasi ya lectio
divina, bali inaidai na kuistawisha. Lakini ikiwa mafumbo yanayozingatiwa
katika Rozari, yakiwa ni pamoja na ukamilisho wake kwa mysteria lucis, yanaishia katika mambo makuu ya maisha ya Kristo,
kutokana nayo roho inaweza kwa urahisi zaidi kuenea katika sehemu nyingine za
Injili, hasa Rozari inaposaliwa katika nafasi maalumu za kujikusanya kirefu
zaidi.
Kusikiliza Neno la Mungu
Ili tafakuri ipewe
msingi wa Kibiblia na udhati mkubwa zaidi, inafaa baada ya kutaja fumbo kuwe na
tangazo la dondoo la Biblia linalohusika ambalo linaweza kuwa refu kadiri ya
hali. Kwa kuwa maneno mengine hayafikii kamwe nguvu maalumu ya Neno lililovuviwa
na Mungu. Hilo linatakiwa kusikilizwa kwa hakika ya kwamba ni Neno lake
lililotamkwa kwa ajili ya leo na «kwa ajili yangu».
Likipokewa hivyo,
linaingia katika mbinu ya kukariri ya Rozari bila ya kusababisha ukinaifu
unaoweza ukatokana na kukumbusha tu habari inayojulikana sana. Hapana, kazi si
kukumbuka habari, bali kuacha Mungu ‘aseme’. Katika nafasi fulani ya fahari na
ya kijumuia inaweza ikafaa Neno hilo lifafanuliwe kifupi.
Kimya
31. Usikivu na tafakuri
vinajilisha kimya. Inafaa kwamba, baada ya kutaja fumbo na kutangaza Neno,
tutulie kwa muda wa kufaa ili kulikazia macho fumbo la kufikiriwa, kabla
hatujaanza sala ya midomo. Kuvumbua upya thamani ya kimya ni siri mojawapo ya
utekelezaji wa sala hasa na wa tafakuri. Kati ya kasoro za jamii iliyotawaliwa
na teknolojia na vyombo vya habari, mojawapo ni kwamba kimya kinazidi kuwa
kigumu. Kama vile katika liturujia zinapendekezwa nafasi za kimya, hata katika
kusali Rozari inafaa nafasi fupi ya kutulia baada ya kulisikiliza Neno la
Mungu, wakati roho inapolenga yaliyomo katika fumbo maalumu.
«Baba
Yetu»
Baada ya kusikiliza
Neno na kulenga fumbo, hakuna budi kujiinua kwa Baba. Yesu, katika kila fumbo
lake, anatufikisha daima kwa Baba, anayemuelekea mfululizo, kwa kuwa ametulia
'kifuani' pake (taz. Yoh 1:18). Yeye anataka kutuingiza katika urafiki wa dhati
na Baba, ili tuseme pamoja naye «Aba!, Baba» (Rm 8:15; Gal 4:6). Ni katika
uhusiano na Baba kwamba yeye anatufanya kuwa ndugu zake na ndugu sisi kwa sisi,
akitushirikisha Roho ambaye ni wa kwake na wa Baba kwa pamoja. Sala ya Baba
Yetu, ikiwekwa kama msingi fulani wa tafakuri juu ya Kristo na Maria inayostawi
kwa njia ya kukariri Salamu Maria, inafanya tafakuri hiyo ya fumbo kuwa
mang’amuzi ya Kikanisa hata inapofanyika upwekeni.
«Salamu
Maria» kumi
33.
Ndiyo sehemu kubwa zaidi ya Rozari na papohapo ndiyo inayoifanya iwe sala ya
Kimaria kwa namna ya pekee. Lakini ikieleweka vizuri Salamu Maria yenyewe
inaonyesha wazi kwamba sifa hiyo ya Kimaria haipingani na sifa ya Rozari kuwa
sala ya Kikristo, bali inaisisitiza na kuikuza. Kwa kuwa sehemu ya kwanza ya
Salamu Maria, inayotokana na maneno ambayo Maria aliambiwa na malaika Gabrieli
na mtakatifu Elizabeti, ni kuzama kwa ibada katika fumbo lililofanyika katika
Bikira wa Nazareti. Tunaweza kusema yanatokeza mshangao wa mbingu na dunia na
kwa namna fulani yanadokeza furaha ya Mungu mwenyewe akitazama uzuri wa kazi yake
bora kuliko zote – umwilisho wa Mwana katika tumbo la kibikira la Maria -,
kufuatana na mtazamo mfurahivu wa kitabu cha Mwanzo (taz. Mwa 1:31), na ile
aina ya ono asili au «pathos ambayo
Mungu, mwanzoni mwa uumbaji, aliitazama kazi ya mikono yake». Katika Rozari,
kukariri Salamu Maria kunatushirikisha furaha hiyo ya Mungu: ni shangwe, ni
mshangao, ni uvumbuzi wa muujiza mkubwa kuliko yote iliyofanyika katika
historia. Ndivyo unavyotimia utabiri wa Maria: «Tokea sasa vizazi vyote
wataniita mbarikiwa» (Lk 1:48).
Kiini cha Salamu Maria,
na kama bawaba kati ya sehemu yake ya kwanza na ya pili, ni jina la Yesu.
Pengine, katika kukariri harakaharaka, kiini hicho kinasahauliwa pamoja na uhusiano
wake na fumbo la Kristo linalokaziwa macho. Lakini mkazo juu ya jina la Yesu na
juu ya fumbo lake ndio unaobainisha matumizi ya Rozari yenye maana na ya kuzaa
matunda. Paulo VI katika himizo la kitume Marialis
Cultus alikumbusha tayari desturi inayofuatwa sehemu fulanifulani ili kutia
maanani jina la Kristo, yaani kuliongezea maneno yanayodokeza fumbo
linalotafakariwa. Ni desturi inayostahili sifa, hasa katika sala ya pamoja.
Inatokeza kwa nguvu imani katika Kristo ikiihusisha na nafasi mbalimbali za
maisha ya Mkombozi. Ni ungamo la imani na, kwa wakati huohuo, inasaidia
kudumisha uzingatifu wa tafakuri, ikiwezesha kulishiza fumbo la Kristo kadiri
ya lengo la kukariri Salamu Maria. Kukariri jina la Yesu – jina pekee ambalo
linatunawezesha kutumaini wokovu (taz. Mdo 4:12) – pamoja na lile la Mama yake
mtakatifu sana, na kama kwa kuacha Maria awe ndiye anayelipendekeza kwetu, ni
safari ya kulishiza inayolenga kutuingiza kwa dhati zaidi na zaidi katika
maisha ya Kristo.
Kutokana na fungamano
lake la pekee kabisa na Kristo, linalomfanya Maria awe Mama wa Mungu, Theotokos, inapata nguvu ile dua ambayo
tunamuelekea katika sehemu ya pili ya sala, tukiyakabidhi maombezi yake ya
kimama maisha yetu na saa ya kufa kwetu.
«Atukuzwe»
Kadiri tafakuri juu ya
fumbo ilivyokuwa zingatifu, ya dhati na kuhuishwa na upendo kwa Kristo na kwa
Maria – Salamu baada ya Salamu – basi kuutukuza Utatu mwishoni mwa makumi,
badala ya kuwa hatima fupi tu, kunapata tuni yake halisi ya kuzama katika
fumbo, kama kwa kuinua roho hadi juu mbinguni na kutufanya kwa namna fulani
tupate sisi pia mang’amuzi ya Tabori, utangulizi wa kuzama kesho katika fumbo:
«Ni vizuri sisi kuwapo hapa» (Lk 9:33).
Sala ya mwisho
Katika kawaida ya
Rozari, baada ya kuutukuza Utatu inafuata antifona iliyo tofauti kadiri ya
desturi. Bila ya kupunguza thamani ya maombi hayo, inafaa tuseme kuwa kuzama
katika mafumbo kunaweza kutokeza vizuri zaidi uwezo wake wa kuzaa matunda
kukiwa na mbinu ya kumalizia kila fumbo kwa sala ambayo ilenge kupata matunda
maalumu ya tafakuri ya fumbo husika. Hivyo Rozari itaweza kutokeza kwa nguvu
zaidi uhusiano wake na maisha ya Kikristo. Kufanya hivyo kunapendekezwa na sala
nzuri ya liturujia inayotualika kuomba kwamba kwa kutafakari mafumbo ya Rozari,
tuweze «kuiga yaliyomo na kupata yanayoahidi».
Hiyo sala ya mwisho
inaweza kufuata namna tofauti halali, kama inavyotokea tayari. Hivyo Rozari
inapata pia sura ya kulingana zaidi na mapokeo mbalimbali ya Kiroho na jumuia
mbalimbali za Kikristo. Katika mtazamo huo, inatarajiwa kwamba yaenee kadiri ya
busara ya kichungaji mapendekezo ya maana zaidi, afadhali kisha kujaribiwa
katika vituo na patakatifu pa Maria ambapo sala ya Rozari inazingatiwa zaidi,
hivi kwamba Taifa la Mungu liweze kufaidika na utajiri wowote halisi wa Kiroho,
likiufanya uwe lishe kwa sala yake hasa.
Tasbihi
Chombo cha mapokeo
cha kusalia Rozari ni tasbihi. Katika matumizi ya kijuujuu zaidi inaishia mara
nyingi kuwa kifaa tu cha kuhesabia Salamu Maria zinazofuatana. Lakini inafaa
pia kutokeza ishara inayoweza kuchangia tena kuzama katika mafumbo. Kuhusu
jambo hilo, neno la kwanza la kusema ni kuwa tasbihi inamuelekea Msulubiwa,
ambaye kwa namna hiyo anafungua na kufunga njia yenyewe ya sala. Maisha na sala
ya waamini kiini chake ni Kristo. Yote yanatoka kwake, yote yamamlenga yeye,
yote kwa njia yake, katika Roho Mtakatifu, yanamfikia Baba.
Kama chombo che
kuhesabia, kinachoonyesha maendeleo ya sala, tasbihi inadokeza safari
isiyokwisha ya sala hasa na ya ukamilifu wa Kikristo. Mwenye heri Bartolo Longo
aliiona pia kama ‘mnyororo’ inayotuunganisha na Mungu. Naam, mnyororo, lakini
mtamu; ndivyo unavyojidhihirisha daima uhusiano na Mungu aliye Baba. Mnyororo
‘wa kitoto’, unaotulinganisha na Maria, «mjakazi wa Bwana» (Lk 1:38), na,
kimsingi zaidi, na Kristo mwenyewe ambaye, ingawa ni Mungu, alijifanya
«mtumishi» kwa kutupenda. (Fil 2:7).
Ni vizuri pia kueneza
maana ya kiishara ya tasbihi upande wa mafungamano kati yetu wenyewe,
tukikumbuka kwa njia yake uhusiano wa ushirika na udugu unaotuunganisha wote na
Kristo.
Mwanzo na mwisho
Kwa sasa katika
mazingira tofauti ya Kanisa kuna namna mbalimbali za kuanza Rozari. Katika
maeneo kadhaa kawaida ni kuanza na dua ya Zaburi 70: «Ee Mungu, uniokoe, Ee
Bwana, unisaidie hima», kama kwa kuchochea ndani ya anayesali hakika nyenyekevu
ya unyonge wake; kumbe pengine mwanzo unafanyika kwa kutamka maneno ya
Nasadiki, kama kwa kuweka ungamo la imani kuwa msingi wa safari ya sala
inayoanza. Namna hizo na nyinginezo ni halali vilevile kadiri zinavyoandaa roho
kuzama katika mafumbo. Halafu sala inafungwa na ombi kwa ajili ya nia za Baba
Mtakatifu, ili kupanua mtazamo wa anayesali hadi upeo mkubwa wa mahitaji ya
Kanisa. Ni kwa ajili ya kuhamasisha mtazamo huo wa Kikanisa wa Rozari, kwamba
Kanisa limeamua kuitajirisha kwa rehema takatifu kwa manufaa ya anayeisali kwa
misimamo yanayotakiwa.
Kwa kweli, Rozari
ikisaliwa hivyo inakuwa kwa hakika safari ya Kiroho ambamo Maria anajifanya
Mama, mwalimu, kiongozi na kumtegemeza mwamini kwa maombezi yake ya nguvu.
Haiwezekani kushangaa kwamba roho, mwishoni mwa sala hiyo, ambapo imeng’amua
kwa dhati umama wa Maria, inajisikia haja ya kumsifu Bikira mtakatifu kwa sala
nzuri ajabu ya Salamu Malkia na kwa Litania ya Loreto. Ni kilele cha safari ya
ndani iliyomleta mwamini karibu sana na fumbo la Kristo na la Mama yake
mtakatifu sana.
Mgawanyo
katika siku za wiki
Rozari inaweza kusaliwa nzima kila siku, na wapo ambao wanafanya hivyo na
kustahili sifa. Hivyo inakuja kujaza kwa sala siku za waaamini wengi
waliojitosa kusali tu, au inakuja kuongozana na wagonjwa na wazee ambao wana
muda mwingi usio na shughuli. Lakini ni wazi kwamba – hasa ukiongezwa mfululizo
mpya wa mysteria lucis – wengi
hawataweza kusali zaidi ya sehemu moja, kadiri ya mpangilio fulani katika wiki.
Mgawanyo huo katika juma unazipatia siku za wiki ‘rangi’ fulani ya Kiroho,
kidogo kama liturujia inavyofanya na vipindi mbalimbali vya mwaka wa Kanisa.
Kadiri ya desturi ya
sasa, Jumatatu na Alhamisi zinatumika kutafakari «mafumbo ya furaha», Jumanne
na Ijumaa «mafumbo ya uchungu», halafu Jumatano, Jumamosi na Jumapili «mafumbo
ya utukufu». Tuingize wapi «mafumbo ya mwanga»? Tukizingatia kwamba mafumbo ya
utukufu yanapendekezwa mfululizo Jumamosi na Jumapili, na kwamba kimapokeo
Jumamosi ni siku ya Maria hasa, inafaa kushauri kuhamishia Jumamosi tafakuri ya
pili ya wiki juu ya mafumbo ya furaha, ambamo uwepo wa Maria unajitokeza. Hivyo
Alhamisi inabaki na nafasi kwa kutafakari mafumbo ya mwanga.
Hata hivyo elekezo hilo
halikusudii kuzuia uhuru wa kufaa katika kutafakari kwa mtu mmojammoja au
kijumuia, kadiri ya mahitaji ya Kiroho na ya kichungaji na hasa kadiri ya
kutukia siku za liturujia ambazo zinaweza zikashauri kurekebisha mpangilio huo
kwa namna ya kufaa. Kilicho muhimu kweli ni kwamba Rozari itazamwe na
kung’amuliwa zaidi na zaidi kama safari ya kuzama katika mafumbo. Kwa njia yake
na kwa kukamilishana na kazi ya liturujia, juma la Mkristo linalotegemea Siku
ya Bwana, siku ya ufufuko, linakuwa safari kupitia mafumbo ya maisha ya Kristo,
naye anajitokeza katika maisha ya wanafunzi wake kuwa ndiye Bwana wa nyakati na
wa historia.
HATIMA
«Rozari
mbarikiwa wa Maria, mnyororo mtamu unaotuunganisha na Mungu»
39. Tuliyoyasema mpaka
sasa yanatokeza sana utajiri wa sala hiyo ya kimapokeo ambayo ina usahili wa
sala ya watu wadogo, lakini pia udhati wa kiteolojia wa sala inayowafaa
wanaojisikia haja ya sala iliyokomaa zaidi.
Daima Kanisa limekiri
kwamba sala hiyo ina nguvu ya pekee, likiyakabidhi matumizi yake ya pamoja na
ya kudumu mambo magumu zaidi. Wakati ambapo Ukristo wenyewe ulikuwa hatarini,
Kanisa liliona kwamba nguvu ya sala hiyo ndiyo iliyoepusha janga, na Bikira wa
Rozari alisalimiwa kama mwombezi wa wokovu huo.
Leo naikabidhi kwa radhi
nguvu ya sala hiyo – kama nilivyodokeza mwanzoni – kipeo cha amani duniani na
kile cha familia.
Amani
Matatizo
yanayojitokeza katika upeo wa ulimwengu mwanzoni mwa milenia mpya yanatufanya
tufikirie wamba kazi kutoka Juu tu, yenye uwezo wa kuelekeza mioyo ya
wanaoishi katika nafasi za kushindana na ya wanaoshika mikononi mwao kesho ya
mataifa, inaweza kutumainisha kwamba kesho hiyo haitakuwa na magiza makubwa
kama ya sasa.
Rozari ni sala ambayo
kwa maumbile yake inalenga amani, kwa sababu ni kumkazia macho Kristo, Mfalme
wa amani na «amani yetu» (Ef 2:14). Anayelifanya fumbo la Kristo kuwa lake pia
– na ndilo lengo hasa la Rozari -, anajifunza siri ya amani na kuigeuza kuwa
mpango wa maisha. Tena, kutokana na tabia yake kama tafakuri, pamoja na
mfuatano wake mtulivu wa Salamu Maria, Rozari inamtuliza anayesali na kumuandaa
kupokea na kung’amua ndani kabisa mwa nafsi yake, halafu kueneza kandokando
yake, ile amani halisi ambayo ni zawadi maalumu ya Mfufuka (taz. Yoh 14:27;
20:21).
Pia ni sala ya amani
kutokana na matunda ya upendo inayoyazaa. Ikisaliwa vizuri kama tafakuri
halisi, Rozari, kwa kurahisisha mkutano na Kristo katika mafumbo yake,
inatambulisha pia uso wa Kristo katika ndugu, hasa wanaoteseka zaidi. Inawezekanaje
kulikazia macho, katika mafumbo ya furaha, fumbo la Mtoto aliyezaliwa
Bethlehemu bila ya kujisikia hamu ya kupokea, kutetea na kustawisha uhai, kwa
kubeba mateso ya watoto sehemu zote za dunia? Inawezekanaje kufuata nyayo za
Kristo mfunuaji wa ukweli, katika mafumbo ya mwanga, bila ya kuazimu kutoa
ushahidi wa Heri zake katika maisha ya kila siku? Tena inawezekanaje kumkazia
macho Kristo aliyelemewa na msalaba na kusulubiwa, bila ya kujisikia haja ya
kumsaidia kama «Wakirene» wake katika kila ndugu aliyevunjwa na uchungu au
kulemewa na hali ya kukata tamaa? Hatimaye, inawezekanaje kuukazia macho
utukufu wa Kristo mfufuka na wa Maria aliyetawazwa Malkia, bila ya kujisikia
hamu ya kufanya ulimwengu huu uwe mzuri zaidi, wenye haki zaidi na kulingana
zaidi na mpango wa Mungu?
Basi, Rozari huku
ikitufanya tumkazie macho Kristo, inatufanya pia wajenzi wa amani duniani. Kwa
sifa yake ya kuwa dua inayosisitizwa na ya pamoja, kulingana na mwaliko wa
Kristo wa kusali «sikuzote» bila ya kukata tamaa (Lk 18:1), inatuwezesha
kutumaini kwamba, leo pia 'pambano' gumu kama lile la amani linaweza kupata
ushindi. Mbali na kukimbia matatizo ya ulimwengu, Rozari inatusukuma hivyo
kuyatazama kwa macho ya uwajibikaji na ya ukarimu, na inatupatia nguvu ya
kuyakabili tukiwa na hakika ya kupata msaada wa Mungu na nia imara ya
kuushuhudia katika nafasi yoyote «upendo, ndio kifungo cha ukamilifu» (Col
3:14).
Familia:
wazazi
Rozari, pamoja na
kuwa sala kwa ajili ya amani, tangu mwanzo ni pia sala ya familia na kwa ajili
ya familia. Zamani sala hiyo ilipendwa sana na familia za Kikristo, na bila ya
shaka ilichangia umoja wake. Ni lazima tusitapanye urithi huo wa thamani. Ni
lazima turudi kusali katika familia na kusali kwa ajili ya familia, kwa kutumia
tena namna hii ya kusali.
Ikiwa katika barua ya
kitume Novo Millennio Ineunte
nilihimiza Liturujia ya Vipindi liadhimishwe na walei pia katika maisha ya
kawaida ya jumuia za parokia na za vyama mbalimbali vya Kikristo, nataka
kufanya vilevile kuhusu Rozari. Ni njia mbili za sala hasa ya Kikristo, si za
kuchagua kati yake, bali za kukamilishana. Hivyo naomba wanaoshughulikia
uchungaji wa familia wahamasishe kwa moyo sala ya Rozari.
Familia inayosali kwa
umoja, inadumu kuwa na umoja. Kwa mapokeo ya muda mrefu, Rozari takatifu inafaa
kwa namna ya pekee kuwa sala inayokusanya familia. Wanafamilia, kwa kumkazia
macho Yesu, wanajipatia upya uwezo wa kutazamana daima usoni ili kuelewana, ili
kushikamana, ili kusameheana, ili kuanza upya kwa agano la upendo lililofanywa
upya na Roho wa Mungu.
Matatizo mengi ya
familia za kisasa, hasa katika jamii zilizoendelea kiuchumi, yanatokana na
kwamba inazidi kuwa vigumu kushirikishana. Kukaa pamoja kunashindikana, na
huenda nafasi chache za kukaa pamoja zikajazwa na picha za televisheni. Kuanza
upya kusali Rozari katika familia ni kuingiza katika maisha ya kila siku picha
tofauti sana, zile za fumbo linalookoa: picha ya Mkombozi, picha ya Mama yake
mtakatifu sana. Familia ambayo inasali pamoja Rozari inaiga kidogo mazingira ya
nyumba ya Nazareti: Yesu anawekwa katikati, kwa kushiriki pamoja naye furaha na
uchungu, kwa kumkabidhi mikononi mahitaji na matarajio, kwa kuchota kwake
tumaini na nguvu ya kuendelea na safari.
...
na watoto
Ni pia jambo zuri na
la kufaa kuikabidhi sala hiyo safari ya kukua kwa watoto. Je, Rozari si safari
ya maisha ya Kristo, tangu kutungwa mpaka kufa, hadi kufufuka na utukufu? Leo
inazidi kuwa vigumu kwa wazazi kuwafuata watoto katika hatua mbalimbali za
maisha. Katika jamii ya teknolojia iliyostawi, ya vyombo vya upashanaji habari
na ya utandawazi, yote yamekuwa yanakwenda haraka sana, na umbali wa
kiutamaduni kati ya vizazi unazidi kukua. Mapema aina yoyote ya ujumbe na
mang’amuzi yasiyotarajiwa yanapata nafasi katika maisha ya watoto na vijana,
hivi kwamba pengine wazazi wanafadhaika kuwaepusha na hatari wanazokabiliana
nazo. Si kwa nadra wanapatwa na hali ya kuvunjika moyo kabisa, wakiona wanao
walivyoshindwa na udanganyifu wa dawa za kulevya, na mivuto ya anasa isiyo na
mipaka, na vishawishi vya ukatili, na aina mbalimbali za matendo yanayotokeza
mtu asivyoona maana ya maisha na alivyokata tamaa.
Kusali Rozari kwa ajili
ya watoto, tena afadhali pamoja na watoto, kwa kuwalea tangu utotoni kuwa na
nafasi hiyo ya «kutulia kwa sala» kifamilia kila siku, bila ya shaka si utatuzi
wa matatizo yote, lakini ni msaada wa Kiroho wa thamani. Inawezekana kupinga
kwa kusema Rozari inaonekana ni sala isiyofaa kuwaridhisha watoto na vijana wa
leo. Lakini pengine hoja hiyo inategemea namna ya kusali ambayo mara nyingi si
sahihi. Zaidi ya hayo, bila ya kupotosha muundo wake wa msingi, hakuna
kinachozuia kwamba kwa watoto na vijana– katika familia kama vile katika
vikundi - sala ya Rozari isitajirishwe na ishara na vitendo vya kufaa, ambavyo
visaidie kuielewa na kufaidika nayo. Kwa nini tusijaribu? Kwa msaada wa Mungu,
uchungaji wa vijana usiokata tamaa bali wenye bidii na ubunifu unaweza kufanya
mambo ya maana kweli. Siku za Kimataifa za Vijana zimenionyesha kiasi gani! Rozari
ikipendekezwa vizuri, nina hakika kuwa vijana wenyewe wataweza kuwashangaza
tena wazee kwa kuifanya sala hiyo kuwa ya kwao na kuitumia kwa umotomoto
maalumu wa umri wao.
Rozari, hazina ambayo tuivumbue upya
Wapendwa ndugu wa
kiume na wa kike! Sala rahisi hivi, na kwa wakati huohuo tajiri hivi,
inastahili kweli kuvumbuliwa tena na jumuia ya Kikristo. Tufanye hivyo hasa
mwaka huu, tukipokea pendekezo hilo kama uimarishaji wa mpango uliochorwa
katika barua ya kitume Novo Millennio
Ineunte, ambayo programu za kichungaji za Makanisa maalumu mengi zimeifuata
katika kupanga juhudi kwa miaka ya jirani.
Kwa namna ya pekee
nawaelekea nyinyi, wapendwa ndugu katika uaskofu, mapadri na mashemasi, nanyi
watenda kazi wa kichungaji katika huduma mbalimbali, ili kwa kung’amua wenyewe
uzuri wa Rozari, muihamasishe kwa bidii.
Nawategemea
nyinyi pia wanateolojia, ili kwa masomo yenu makini na ya hekima kwa wakati
mmoja, yenye mzizi katika Neno la Mungu na usikivu kwa maisha halisi ya taifa
la Wakristo, mtokeze misingi ya Kibiblia, utajiri wa Kiroho na nguvu ya
kichungaji ya sala hiyo ya kimapokeo.
Nawategemea nyinyi,
wanaume na wanawake mliowekwa wakfu, ambao mnaitwa kwa namna ya pekee kuukazia
macho uso wa Kristo mkijifunza kwa Maria.
Nawaangalia nyinyi nyote,
ndugu wa kiume na wa kike wa hali yoyote ya maisha, nyinyi, familia za
Kikristo, nanyi wagonjwa na wazee, nanyi vijana: mshike upya mikononi kwa
tumaini tasbihi ya Rozari, mkiivumbua upya katika mwanga wa Maandiko
matakatifu, kulingana na liturujia, katika hali halisi ya maisha ya kila siku.
Mwaliko wangu huu
usipotee bure! Mwanzoni mwa mwaka wa ishirini na tano wa upapa wangu, nakabidhi
barua hii ya kitume mikononi mwa Bikira Maria mwenye hekima, nikisujudu Kiroho
mbele ya picha yake iliyopo katika patakatifu pazuri ajabu ambapo mwenye heri
Bartolo Longo, mtume wa Rozari, alipajenga kwa heshima yake. Najitwalia kwa
radhi maneno yake ya kusisimua ambayo alifunga Dua maarufu kwa Malkia wa Rozari
takatifu: «Rozari mbarikiwa wa Maria, mnyororo mtamu unaotuunganisha na Mungu,
kiungo cha upendo kinachotuunganisha na Malaika, mnara wa wokovu dhidi ya
mashambulizi ya toka motoni, bandari salama katika dhoruba iliyotupata sote,
sisi hatutakuacha tena kamwe. Wewe utatufariji saa ya kufa. Kwako tutatoa busu
la mwisho uhai utakapozimika. Na sauti ya mwisho ya midomo yetu itakuwa jina
lako tamu, Malkia wa Rozari wa Pompei, Mama yetu mpendwa, kimbilio la wakosefu,
Mtawala mfariji wa wenye huzuni. Uhimidiwe popote, leo na daima, duniani na
mbinguni».
Kutoka Vatikano, tarehe
16 Oktoba mwaka 2002, mwanzo wa mwaka wa ishirini na tano wa Upapa wangu.
0 comments:
Post a Comment