Home » » BIKIRA MARIA KATIKA BIBLIA

BIKIRA MARIA KATIKA BIBLIA


MAANDIKO YANASHUHUDIA UMUHIMU WA WATU UNAOTOFAUTIANA

Maandiko matakatifu yanawasifu watu mbalimbali kutokana na walivyomuamini Mungu na kutenda makuu kwa ajili ya taifa lake. Abrahamu alimuamini na kuwa tayari kumtolea sadaka mwanae Isaka, tukio lililomfanya apate baraka ya pekee ya kuwa baba wa waamini (Mwa 22:15-18). Yosefu, kipenzi wa Yakobo, alikuwa mwaminifu hata akaliokoa taifa lisiangamie kwa njaa (Mwa 50:20). Musa ndiye mkombozi wa taifa la Mungu katika Agano la Kale: aliongoza Israeli kutoka utumwani Misri akalipatia sheria kutoka kwa Mungu katika mlima Sinai. Maandiko ya Agano la Kale yanakiri, “Wala hajainuka kiongozi kama alivyokuwa Musa” (Kumb 34:10-12). Kwa kuwa watu hao ni wengi mno tunaorodhesha wafuatao: Yoshua, Debora, Gideoni, Samsoni, Samweli, Ruthu, wafalme Daudi na Solomoni, manabii Eliya, Yeremia na Ezekieli. Nabii Isaya ana sifa ya pekee katika kumchora Masiya. Mwishoni Bwana Yesu mwenyewe anamsifu Yohane Mbatizaji akisema, “Ni mkuu kati ya uzao wa wanawake” (Lk 7:24-28). Bikira Maria ana nafasi gani kati yao? Hao tuliowataja walitenda kweli mambo makuu kwa imani, lakini Bikira Maria yuko juu sana kupita hao wote, tena kwa mbali: yeye ni malkia wa makundi yote ya mbinguni, sio ya watu tu, bali hata ya malaika. Mapokeo ya mashariki humuita “daraja linalounganisha dunia na mbingu”, “mfano aliouona Yakobo” (Mwa 28:12).


BIKIRA MARIA KATIKA BIBLIA
UTABIRI KUHUSU BIKIRA MARIA, EVA MPYA

Mapokeo yamtazama Bikira Maria kama Eva mpya atakayemshinda nyoka wa kale (Ibilisi). Kwa nini Eva mpya? Kwa sababu Eva wa kale alidanganywa na kuangushwa na Shetani, hivyo alitenda dhambi. Kumbe Maandiko matakatifu yanatupatia utabiri kuhusu Eva mpya atakayemshinda adui (Shetani) kwa kumponda kichwa: “Nitaweka uadui kati yako na huyu mwanamke, kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa chako” (Mwa 3:15). “Tazama Bikira atachukua mimba, atazaa mtoto mwanamume, naye atamuita jina lake Emanueli, yaani Mungu pamoja nasi” (Isa 7:14). Dondoo hilo lilinganishwe na Lk 1:34-35, “Mariamu akamwambia malaika, Litakuwaje neno hili, maana sijui mume? Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu akakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli. Kwa sababu hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu”. Utabiri mwingine wasema, “Litatoka chipukizi katika shina la Yese, na tawi litakalotoka katika mizizi yake litazaa matunda. Na Roho wa Bwana atakaa juu yake, Roho ya hekima na ufahamu, Roho wa shauri na uwezo, Roho wa maarifa na ya kumcha Bwana” (Isa 11:1-2). Je, shina hilo si yeye Mama Bikira Maria, na tawi alilochipusha si Mwanae Bwana wetu Yesu Kristo? “Umebarikiwa wewe katika kila hema la Yuda na katika kila taifa, nao wanaposikia jina lako watafadhaika. Imani yako haitatoka mioyoni mwa watu wanaoukumbuka uweza wa Mungu milele” (Yudithi 14:7; 15:9).
Linganisha dondoo hili na Lk 1:42, “Akapaza sauti kwa nguvu akasema, Umebarikiwa wewe kuliko wanawake wote, na yeye utakayemzaa amebarikiwa”. Je, utasema Bikira Maria ni mtu wa ziada katika mpango wa Mungu? Tena tunasoma, “Imba, ee binti Sion, piga kelele, ee Israeli, furahi na kushangilia kwa moyo wako wote, ee binti Yerusalemu. Mfalme wa Israeli, naam, yeye Bwana yu katikati yako” (Sef 3:14-15). Linganisha dondoo hilo na
Injili: “Malaika akaingia nyumbani mwake akamwambia, Furahi Maria, umejaliwa neema kubwa, Bwana yu pamoja nawe” (Lk 1:28).

BIKIRA MARIA KATIKA AGANO JIPYA
Mambo yaliyotabiriwa katika Agano la Kale yametimia katika Agano Jipya: ukombozi wetu ulianza pale Bikira Maria alipokubali fumbo la umwilisho wa Mwana wa Mungu, akisema kwa hiari, “Mimi ni mtumishi wa Bwana, na
iwe kwangu kama ulivyonena” (Lk 1:38). Je, Bikira Maria ni bahasha? Siku hizi kuna baadhi ya waheshimiwa ambao wanadhani kujua Maandiko kuliko
watu wengine, tena wanadai wanaye Roho Mtakatifu; kumbe wanadiriki kumuita Mama huyo mtakatifu, eti ni “bahasha” ambayo ikileta barua haina kazi! Jambo hili linasikitisha sana na sio tu kumkosea heshima Mama yetu
mpendwa wa mbinguni, bali inaweza pia kuwa kufuru kwa Mwenyezi Mungu aliyemuumba kama msaidizi wa Mkombozi aliyejaa neema.
Manabii mbalimbali kwa mwanga wa Roho Mtakatifu walimuagua kwa heshima; Mama Elizabeti alijiona hastahili kutembelewa naye akamuita, “Mama wa Bwana wangu”; mzee Simeoni alimuagulia mateso yenye uchungu kama upanga yatakayopenya moyowe. Bwana Yesu aliyefurika Roho Mtakatifu tangu nukta ya kuchukuliwa mimba, wakati alipokaribia kufa pale msalabani alimuita, “Mama”; jumuia ya Mitume na wafuasi wa kwanza walimtaja kipekee ilivyo ishara ya heshima. Je, Roho Mtakatifu ndiye anayewaongoza hawa ndugu zetu wamuite bahasha? Je, ni Roho yuleyule aliyewaongoza Mitume na manabii ama roho ya aina nyingine? “Wapenzi wangu, msisadiki kila mtu asemaye kwamba ana Roho wa Mungu, bali chunguzeni kwa makini kama huyo mtu anaongozwa na Roho wa Mungu au la, maana manabii wengi wa uongo wamezuka ulimwenguni” (1Yoh 4:1).
Bikira Maria sio “chombo” tu, bali mshiriki wa kazi ya ukombozi ya Mwanae. Kadiri ya mtume Paulo kuteseka ni kutimiliza yaliyopungua katika mateso ya Kristo kwa ajili ya Kanisa, “Na sasa nafurahi kuteseka kwa ajili yenu,
maana kwa mateso yangu hapa duniani nasaidia kukamilisha kile kilichopungua bado katika mateso ya Kristo” (Kol 1:24). “... maana tukiyashiriki mateso yake Kristo, tutaushiriki pia utukufu wake” (Rom 8:17b). Katika hilo la
kumfuata Mwanae katika mateso Bikira Maria alitabiriwa wazi na mzee Simeoni, “Tazama huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa. Nawe mwenyewe uchungu ulio kama
upanga utauchoma moyo wako” (Lk 2:34-35). Bikira Maria alishiriki mateso ya ukimbizi huko Misri kwa lengo la kumficha Mwanae asiteswe na Herode, “Hivyo Yosefu aliamka akamchukua mtoto pamoja na Mama yake akaondoka usiku akaenda Misri akakaa huko mpaka Herode alipokufa” (Math 2:14-15).

BIKIRA MARIA MWOMBEZI KATIKA HARUSI YA KANA:
Mama Bikira Maria anaonekana mwenye kuonea huruma wenye shida: kwa ombi lake huko Kana ya Galilaya Yesu aligeuza maji kuwa divai, na wanafunzi wake wakamwamini (Yoh 2:1-12).

BIKIRA MARIA AFANYWA EVA MPYA:
Juu ya Eva wa zamani imesemwa ni Mama wa walio hai: “Adamuakamwita mkewe jina lake Hawa, kwa kuwa ndiye aliye Mama wa walio hai” (Mwa 3:20). Hata hivyo Agano Jipya linaonyesha Adamu na Eva wa zamani wametuletea kifo (Rom 5:12). Yesu, aliye Adamu mpya, alipokuwa anakamilisha sadaka ya ukombozi pale msalabani alimfanya Bikira Maria awe Eva mpya kwa kitendo cha kumkabidhi mwanafunzi, tena yule aliyempenda zaidi. “Basi Yesu aipomwona Mama yake na yule mwanafunzi aliyempenda amesiMama karibu akamwambia Mama yake, Mama, tazama Mwanao. Kisha akamwambia yule mwanafunzi, Tazama Mama yako” (Yoh 19:26-27). Zaburi yasema, “Lakini juu
ya Sion itasemwa, Sion ni Mama yao wote; Mungu mkuu ameuthibitisha. Mwenyezi Mungu ataorodhesha mataifa na kuandika juu ya kila moja, Huyu chanzo chake ni Sion” (Zab 87:5-6).

PALE MSALABANI BIKIRA MARIA:
1.   alifanywa Mama wa wote wanaompenda Mwanae;
2.   alifanywa malkia wa wafiadini;
3.   kisha kumzaa pasipo uchungu Bwana wa uzima, pale alituzaa sisi kwa uchungu wa kutisha uliotokana na kumuona Mwanae akifa msalabani. Hata hivyo Bikira Maria aliendelea kumuamini Mwanae aliyeonekana
          ameshindwa;
4.   katika kuteswa kwa Yesu Bikira Maria alishuhudia hatua kwa hatua; wanafunzi wa Yesu walipokimbia na kumtazama kwa mbali, Bikira mtakatifu alikuwa karibu akaona vema kila teso lililompata. Tenakutokana na fungamano la upendo wa ajabu lililokuwepo kati ya Yesu na Mamaye, aliposhuhudia matesoya Mwanae aliteseka sana katika moyo wake safi usio na doa, kiasi kwamba baadhi ya watakatifu
wanasema, Msalaba wa Yesu uliwasulubisha wote, Yesu mwilini na Mama yake moyoni. Uaguzi wa mzee Simeoni ulitimia hivyo.













JE, BIKIRA MARIA ALIZAA WATOTO WENGINE?

Mapokeo kuhusu Bikira Maria yanaonyesha alikuwa binti pekee wa wazee watakatifu Yohakimu na Ana. Vilevile Mt. Yosefu, ingawa kisheria alikuwa mume wake, hakutenda naye tendo la ndoa hata moja. Ndiyo maana kwenye
litania yake tunamuita mwenye usafi kamili. Alikufa kabla Yesu hajaanza utume kwa kubatizwa kwenye mto Yordani. Sisi tunasadiki Maria ni “Bikira daima”. Ndugu wa Yesu wanaosemwa katika Injili ni kina nani? Wanaosemwa katika Injili “ndugu zake Yesu” si watoto wa Bikira Maria wala Yosefu mtakatifu, bali ndugu wa kiukoo waliokuwa jirani sana na familia hiyo takatifu. Kama Bikira Maria angekuwa na watoto wengine, je, Yesu Bwana wetu asingekuwa amefanya kosa la kiudugu kuwanyang’anya Mama yao na kumfanya awe Mama wa mtume Yohane alipomkabidhi msalabani, “‘Mwana, tazama Mama yako’. Na tangu saa ile huyo mwanafunzi alimchukua akae nyumbani kwake” (Yoh 19:27). Katika Agano Jipya yupo Yakobo anayeitwa na mtume Paulo “ndugu yake Bwana” (Gal 1:19): Yakobo huyo alikuwa maarufu katika Kanisa la Yerusalemu (Mdo 12:7; 15:13-21; 21:18-20; Gal 2:9). Yakobo huyo si mtume Yakobo mwana wa Alfayo, wala mtume Yakobo kaka yake Yohane (Lk 6:12-16), bali ni Yakobo ndugu yake Yose na mama yao kwenye Injili anaitwa “Maria mwingine”, si Maria Mama wa Yesu. “Walikuwepo pia wanawake waliotazama kwa mbali. Miongoni mwao akiwa Maria Magdalena, Salome na Maria mama wa akina Yakobo mdogo na Yose” (Mk 15:40). Maria lilikuwa jina la kawaida kwa Wayahudi: akina Maria wakiwa wengi hivyo, tujue
kuwatofautisha kwenye Injili. Bikira Maria Injili zinamtaja kama “Mama wa Yesu”. JE, WAKATI WA KUFANYA UTUME YESU ALIMDHARAU MAMA YAKE? Wengine husoma Maandiko matakatifu wakiishia ujuu bila ya kufikiria wala kulinganisha na mistari mingine. Hivyo hukwazwa na semi kadhaa za Bwana Yesu ambazo kimsingi hazimpingi Mama yake, bali zinampongeza.
“Alipokuwa akisema hayo, mwanamke mmoja katika lile kundi la watu akasema, ‘Hongera kwa mwanamke aliyekuzaa na kukunyonyesha’. Yesu akamjibu, ‘Barabara, lakini heri yake zaidi yule anayelisikia Neno la Mungu na
kulishika’” (Mk 11:27-28). Tena lingine lasema, “Basi, mtu mmoja akamwambia, ‘Mama yako na ndugu zako wako nje, wataka kusema
nawe’. Lakini Yesu akamjibu huyo mtu aliyemwambia hivyo, ‘Mama yangu ni nani, na ndugu zangu ni akina nani?’Kisha akanyosha mkono wake juu y aweanafunzi wake akasema, ‘Hawa ndio Mama yangu na ndugu zangu, maana yeyote anayefanya anavyotaka Baba yangu aliye mbinguni, huyo ndiye kaka yangu na dada yangu na Mama yangu’” (Math 12:46-50).








Je, sehemu hizi za Maandiko zinampinga kweli Bikira Maria au zinampongeza?
Sababu:
  1. Jamaa yake Elizabeti alimpongeza, tena akiongozwa na Roho Mtakatifu,   
     “Heri yako wewe uliyesadiki kwamba yatatimia yale uliyoambiwa na Bwana”    
     (Lk 1:45).
  1. Bikira mtakatifu alipopashwa habari na malaika hakukataa mpango wa    
    Mungu, bali kwa hiari yake alikubali fumbo la mpango wake. “Maria   
    akasema, ‘Mimi ni mtumishi wa Bwana, na iwe kwangu kama ulivyonena’. 
    Kisha malaika yule akaenda zake” (Lk 1:38).
  1. Bwana Yesu alitaka kuwainua wasikilizaji wake wafuate mambo ya Kiroho kuliko ya mwilini. Hivyo ni kweli, Bikira Maria anasifiwa kwanza kwa imani yake, iliyokuwa ya juu zaidi kushinda hata ile ya Abrahamu, kuliko kwa kumchukua Yesu tumboni tu. Hata hivyo tusisahau kuwa Yesu, kama mtu yeyote mcha Mungu, aliwaheshimu wazazi wake, tena tunasikia aliwatii. “Basi, akarudi pamoja nao Nazareti,  akawa anawatii” (Lk 2:51). Naomba, kabla hujahukumu neno moja, angalia ujumla wake. Yesu alizaliwa na Bikira mtakatifu, ndiye aliyemlea na kuhangaika naye huko na huko hata Misri ili kumuepusha na kifo. Ishara ya kwanza kwenye maisha ya hadhara iliyongozwa na Bikira Maria huko Kana. Maria alikuwepo hata wakati wa Yesu kuteswa, akiteseka pamoja naye. Pale msalabani alikabidhiwa Kanisa kwa njia ya Yohane mtume. Bikira Maria alikuwepo hapo mwanzo wa Kanisa, na ndiye aliyelivutia zaidi Roho Mtakatifu kwa njia ya sala yake. “Hao wote walikusanyika pamoja kusali, pamoja na wanawake kadha wa kadha, na Maria Mama yake Yesu na   ndugu zake” (Mdo 1:14).

DOGMA ZA KANISA KUHUSU BIKIRA MARIA

Kuna mafundisho makuu manne kumhusu Bikira Maria ambayo ni lazima kila Mkatoliki ayasadiki kutokana na ufunuo wa Mungu:

1. B. Maria mkingiwa dhambi ya asili
2. B. Maria Mama wa Mungu
3. B. Maria Bikira daima
4. B. Maria kupalizwa mbinguni mwili na roho

MKINGIWA DHAMBI YA ASILI
Tunasadiki Bikira Maria tangu atungwe mimba Mungu alimkinga na kila doa la dhambi kwa kutazamia stahili za Yesu Kristo aliye Mkombozi wa binadamu wote. Ndiye mwanakanisa aliyekombolewa kwa namna bora kushinda
viungo vyote vya Kanisa. Maisha yake yote hakutenda dhambi hata moja. Mapokeo ya mashariki yanamuita A Panagia = Mtakatifu tu. Dogma hiyo ilitangazwa na papa Pius IX mwaka 1854, hata mwaka 1858 Bikira Maria
alijitambulisha huko Lurdi (Ufaransa) kwa Mt. Bernadetta Soubirous kama Mkingiwa. Tena pale Fatima (Ureno) tumefunuliwa moyo wake safi usio na doa.

MAMA WA MUNGU
Injili ya Yohane inaanza kwa kishindo, “Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu” (Yoh 1:1). Huyo Mungu Mwana ndiye aliyetwaa ubinadamu katika Bikira Maria akazaliwa mtoto, jina lake Yesu, maana yake Mungu Mwokozi. Huyo ni binadamu kama sisi isipokuwa hana dhambi. Ubinadamu wa Yesu unategemea Nafsi yake ya Kimungu, hivyo akisema, ‘Mimi’, anamaanisha Nafsi yake ya Kimungu. Ndiyo maana aliwaambia Wayahudi, “Kweli nawaambia, kabla Abrahamu hajazaliwa, nalikuwepo” (Yoh 8:50). “Kama vile Baba alivyo asili ya uhai, ndivyo alivyomjalia Mwanae kuwa asili ya uhai” (Yoh 5:26). Je, Bikira Maria ni Mama wa Mungu tangu lini? Mtume Paulo anaeleza, “Wakati maalumu ulipotimia Mungu alimtuma Mwanae aliyezaliwa na mwanamke” (Gal 4:4). Ni kwanzia wakati huo: sasa imepita miaka 2006 tangu Bikira Maria ajiliwe na sifa hiyo ya kumchukua mimba, kumzaa, kumnyonyesha na kumlea mtu ambaye kwa asili ni  Mungu. Cheo hicho kimemuinua juu kuliko hata malaika, akawa malkia wao. “Malaika alimwambia, ‘Hicho kitakachozaliwa kitaitwa Kitakatifu, Mwana wa Mungu’” (Lk 1:35). Dogma ilitolewa mwaka 431 kwenye Mtaguso wa Efeso uliomuita “Mzazi wa Mungu”.

BIKIRA NA MAMA
Fumbo la Bikira Maria hapa linagongana na akili ya kibinadamu. Wote wanakiri ya kuwa Yesu alimwilishwa bila ya mchango wa mwanamume, kumbe la ajabu zaidi ni kwamba hata uzazi wenyewe haukuondoa ubikira wake, bali uliutakasa. Ingawa akili yetu inakataa, sisi tunakiri na malaika, “Hakuna lisilowezekana kwa Mungu” (Lk 1:38). Ndiyo maana tunamkiri ni Bikira daima.

KUPALIZWA MBINGUNI MWII NA ROHO
Baada ya maisha haya ya duniani Bikira Maria mwenye heri alipalizwa mbinguni mwili na roho, ishara ya mwanamke mshindi. “Ishara kubwa ikaonekana mbinguni, ambapo mwanamke aliyevikwa jua, pia na mwezi chini
ya miguu yake, na taji la nyota kumi na mbili juu ya kichwa chake” (Ufu 12:1).


HESHIMA ZA LITURUJIA KWA MARIA
Kuna ibada za Mama Bikira Maria zinazoadhimishwa katika liturujia. Hapa tunazipanga kulingana na heshima zinavyozidiana:

SHEREHE
a.       8 Desemba – Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili
b.      1 Januari – Bikira Maria Mama wa Mungu
c.       25 Machi – Bikira Maria Kupashwa Habari
d.      15 Agosti – Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni

SIKUKUU
a.       31 Mei – Maamkio ya Bikira Maria
b.      8 Septemba – Kuzaliwa kwa Bikira Maria

KUMBUKUMBU
a.       Juni – Moyo Safi wa Maria
b.      15 Septemba – Mama Yetu wa Huzuni
c.       22 Agosti – Bikira Maria Malkia
d.      7 Oktoba – Bikira Maria wa Rozari
e.       21 Novemba – Bikira Maria Kutolewa Hekaluni

KUMBUKUMBU YA HIARI
a.       11 Februari – Mama Yetu wa Lurdi
b.      16 Julai – Mama Yetu wa Mlima Karmeli
c.       5 Agosti – Kutabaruku wa Kanisa la B. Maria.

Tena kila Jumamosi isiyo na adhimisho maalumu, Kanisa huadhimisha kumbukumbu ya Mama wa Mungu. Pia zipo heshima za binafsi kwa Bikira Maria mwenye heri: mashariki tenzi na nyimbo (k.mf. Akatistos, tenzi za
mt. Efrem shemasi, na nyingine); magharibi (Roma) tunamheshimu binafsi na hata kijumuia kwa kusali rozari takatifu. Ndiyo ibada ya binafsi inayompendeza sana baada ya zile za liturujia hata akatokea sehemu mbalimbali duniani akihimiza tusali rozari ili tupate amani binafsi, kitaifa na kimataifa. Mwezi wa tano ni mwezi wa Maria. Mwezi wa kumi ni mwezi wa Rozari. Mtu aliyeonja matunda ya kumheshimu Maria mtakatifu, Mama wa Mungu, anajua uwezo wa maombezi yake. Kanisa linakiri neema zote za Mungu zaja kwetu kwa njia ya Maria. Je, tunamuabudu Bikira Maria? Hapana, Bikira Maria hatumuabudu hata kidogo, bali tunamtolea heshima ya juu kuliko watakatifu wengine. Mungu tu tunampa heshima ya ‘latria’ (kuabudu), watakatifu tunawaheshimu (dulia) na
Bikira Maria tunampa heshima sana (yuper-dulia). Kweli Mama Bikira Maria ni “kina kisichochunguzika kwa macho ya malaika” (Akatistos). Ni fumbo la ajabu
alilolifanya Mungu katika mpango wa wokovu kwa ajili yake na kwa ajili yetu. Katika Injili ya Yohane Bwana Yesu alisema, “Ninayo bado mengi ya kuwaambieni, ila kwa sasa hamwezi kuyastahimili, lakini atakapokuja huyo Roho wa ukweli atawaongoza kwenye ukweli wote” (Yoh 16:12-13). Kwa msaada wa Roho Mtakatifu heshima kwa Bikira Maria ilienea katika Kanisa lote tangu zamani kabisa. Tena katika Injili ya Luka kuna utabiri wa kumheshimu Bikira Maria vizazi vyote, “Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma mtumishi wake mdogo, hivyo tangu sasa vizazi vyote  wataniita mwenye heri” (Lk 1:48).


http://www.vaticanradio.org/../img_common/x.gif
FUNDISHO LA BIKIRA MARIA KUPALIZWA MBINGUNI MWILI NA ROHO LINAPATA CHIMBUKO LAKE KATIKA IMANI YA KANISA 15/08/2011 13.15.07
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, wakati wa sala ya Malaika wa Bwana, katika maadhimisho ya sherehe ya Bikira Maria kupalizwa mbinguni mwili na roho anasema, fundisho hili la imani lilitolewa na Baba Mtakatifu Pio wa kumi na mbili kunako mwaka 1950, Mama Kanisa alipokuwa anaadhimisha Mwaka wa Imani. Fundisho hili linapata chimbuko lake katika imani ya Kanisa tangu nyakati za karne za mwanzo mwanzo.

Siku kuu hii kwa Kanisa la Mashariki inafahamika kuwa ni "Dormitio" yaani, "Kulala kwa Bikira Maria. Kanisa linaadhimisha kwa shangwe na furaha kupalizwa mbinguni kwa Bikira Maria, akiwa amevikwa jua na mwezi chini ya miguu yake na taji la nyota kumi mbali juu ya kichwa chake. Bikira Maria ni Eva mpya aliyemshinda shetani, kielelezo cha Kristo mshindi dhidi ya dhambi na mauti.

Bikira Maria ametunukiwa zawadi ya kupalizwa mbinguni kutokana na mchango wake katika kazi ya ukombozi. Hiki ni kielelezo cha furaha na matumaini kwa wafuasi wa Kristo, changamoto ya kuwa na ujasiri na imani katika ufufuko wa Kristo.
http://www.vaticanradio.org/../img_common/x.gif
BIKIRA MARIA NI KIELELEZO CHA SANDUKU LA AGANO, UTIMILIFU WA MAPENZI YA MUNGU NA UKWELI KATIKA AGANO LA MILELE KATIKA KRISTO YESU! 15/08/2011 11.01.51
Siku kuu ya Bikira Maria kupalizwa mbinguni mwili na roho ni mwaliko kwa waamini: kumpenda, kumheshimu na kumshangilia kutokana na matendo makuu ambayo Mwenyezi Mungu amemtendea katika maisha yake. Bikira Maria anawasaidia waamini kuona undani wa imani yao: matatizo, matumaini katika mwanga wa hija ya maisha ya kiroho ya Mama wa Mungu, tumaini la wafuasi wote wa Kristo.

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita katika maadhimisho ya Sherehe za Bikira Maria kupalizwa mbinguni mwili na roho, kwenye Kanisa la Mtakatifu Tommaso da Villanova, Parokia ya Castel Gandolfo. Sanduku la Agano ni kielelezo cha uwepo wa Mungu kati ya watu wake. Bikira Maria ni tabernakulo ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili kwa njia ya Roho Mtakatifu, akakaa kati ya watu wake. Katika maisha yake, alijitahidi kuhifadhi moyoni mwake Neno la Mungu, kielelezo cha uaminifu katika utekelezaji wa mapenzi ya Mungu.

Bikira Maria ni kielelezo cha Sanduku la Agano, lililomhifadhi Mwana wa Mungu, utimilifu wa mapenzi ya Mungu na ukweli katika Agano Jipya na la Milele, lililofikia kilele chake kwa kumwaga Damu yake Azizi kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu. Bikira Maria ni Sanduku la Agano la uwepo na upendo wa Mungu, unaojionesha kwa namna ya pekee kwa njia ya Yesu Kristo.

Kutokana na upendeleo wa pekee, aliweza kushiriki pia katika utukufu wa Mwanaye mpendwa Yesu Kristo. Ndiyo maana Mama Kanisa anamwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani. Katika maisha yake, alionesha umuhimu wa kufanya mambo ya Mungu kwa haraka.

Anapomtembelea binamu yake Elizabeth, ndani mwake amembeba Neno wa Mungu, kwa njia ya Roho Mtakatifu, Elizabeth anatambua uwepo wa Mtoto Yesu tumboni mwa Bikira Maria na uwepo wa Mtoto Yohane Mbatizaji tumboni mwake. Kielelezo cha watu wenye haki miongoni mwa Waisraeli na tumaini kwa ujio wa Mkombozi wa ulimwengu.

Kitendo cha Mtoto Yohane Mbatizaji kuruka kwa shangwe tumboni mwa mama yake ni kumtambua Bikira Maria kuwa ni Sanduku la Agano, chemchemi ya furaha inayopaswa kushirikishwa kwa wengi zaidi.

Baba Mtakatifu anasema Bikira Maria aliyepalizwa mbinguni anawafungulia waamini matumaini katika maisha yanayosheheni furaha, anawaonesha njia ya kufuata pamoja na kumpokea Kristo kwa imani na matumaini makuu. Ni mwaliko wa kuendeleza na kudumisha urafiki na Yesu Kristo, licha ya Misalaba, taabu na mahangaiko ambayo waamini wanaweza kukutana nayo katika hija ya maisha yao.

0 comments:

Post a Comment

RICHARD MATANDA TESHA

 
Support : Richie | Bikira Maria | Elimu Endelevu
Copyright © 2013. BIKIRA MARIA - All Rights Reserved
Template Created by Mwariko Published by Mwariko team
Proudly powered by Jicho la Habari